Mazingira FM

Uchakavu wa madarasa na vyoo waitesa Nyasura shule ya msingi

21 May 2026, 7:49 pm

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM kata ya Nyasura, Joseph Msalo CCM

Licha ya Serikali inayoongozwa na CCM kuendelea kuboresha sekta ya elimu nchini, bado Shule ya Msingi Nyasura inahitaji kuangaliwa kwa jicho la pili.

Na Adelinus Banenwa

Wito umetolewa kwa Serikali kuiangalia kwa karibu Shule ya Msingi Nyasura iliyopo Kata ya Nyasura, Halmashauri ya Mji wa Bunda, kutokana na uchakavu mkubwa wa majengo yake pamoja na upungufu wa matundu zaidi ya 40 ya vyoo vya wanafunzi na walimu.

Hayo yamebainishwa wakati wa ziara ya Kamati ya Utekelezaji ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kata ya Nyasura, iliyoongozwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi, Joseph Msalo. Katika ziara hiyo, amesema kuwa licha ya Serikali inayoongozwa na CCM kuendelea kuboresha sekta ya elimu nchini, bado Shule ya Msingi Nyasura inahitaji kuangaliwa kwa jicho la pili ili kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia.

Aidha, amemtaka Diwani wa Kata hiyo pamoja na Mbunge wa eneo husika kufanya jitihada za kuhakikisha shule hiyo inafanyiwa maboresho ya haraka, hususan katika miundombinu ya madarasa na huduma za vyoo kwa wanafunzi na walimu.

Baadhi ya madarasa shule ya msingi nyasura ambayo yamechakaa
Sauti ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM kata ya Nyasura, Joseph Msalo CCM

Awali, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nyasura, Nyabusende Daud, amesema kuwa shule hiyo kwa sasa ina wanafunzi 1,070, ambapo idadi hiyo imepungua baada ya wanafunzi 196 kuhamishiwa katika Shule mpya ya Victoria. Hata hivyo, amesema idadi iliyopo bado ni kubwa kulinganisha na miundombinu iliyopo shuleni hapo.

Aidha, ameiomba Serikali kuboresha mazingira ya shule hiyo ikiwemo ujenzi wa vyoo vya walimu ambavyo kwa sasa havipo kabisa, hali inayosababisha changamoto kubwa kwa walimu pamoja na shughuli za kila siku za shule hiyo.

Sauti ya Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Nyasura, Nyabusende Daud,

Kwa upande wao, baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji waliokuwa wameambatana na mwenyekiti katika ziara hiyo wamesema kuwa pamoja na changamoto zilizobainika katika Shule ya Msingi Nyasura, bado kuna mahitaji mengine muhimu yanayohitaji kufanyiwa kazi katika sekta ya elimu ndani ya kata hiyo.

Wajumbe hao wameiomba Serikali kupitia kwa Diwani wa Kata ya Nyasura kujenga mabweni katika Shule ya Sekondari ya Dkt. Nchimbi, hususan kwa wanafunzi wa kidato cha tano na sita kutokana na umbali mkubwa wanaotoka wanafunzi hao kufuata masomo.

Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji waliokuwa wameambatana na mwenyekiti katika ziara

Aidha, wajumbe hao wameeleza kusikitishwa na hali ya madarasa ya awali katika Shule ya Msingi Victoria kutotumika kutokana na uvamizi wa nyuki. Wamesema hali hiyo inawanyima wanafunzi fursa ya kutumia madarasa hayo licha ya Serikali kuyajenga kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kujifunzia.

Kutokana na changamoto hiyo, wamemuomba Diwani wa kata hiyo kushirikiana na Halmashauri kuhakikisha nyuki hao wanaondolewa haraka ili madarasa hayo yaanze kutumika kama ilivyokusudiwa na Serikali.

Sauti za Baadhi ya wajumbe wa Kamati ya Utekelezaji