Mazingira FM

DC Bunda atoa saa 24 kwa BUWSSA kutatua changamoto ya maji

16 June 2026, 2:54 pm

Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Aswege Enock Kaminyoke

Iwapo mamlaka hiyo haitatekeleza maelekezo hayo ndani ya muda uliopangwa, basi viongozi wa mamlaka hiyo hawana sababu ya kuendelea kubaki Bunda.

Na Adelinus Banenwa

Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Aswege Enock Kaminyoke ametoa maagizo ya saa 24 kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Bunda BUWSSA kuhakikisha wananchi wa Halmashauri ya Mji wa Bunda wanapata huduma ya maji mara moja, kufuatia kuongezeka kwa malalamiko ya muda mrefu kuhusu uhaba wa maji katika maeneo mbalimbali.

Mhe. Kaminyoke amesema iwapo mamlaka hiyo haitatekeleza maelekezo hayo ndani ya muda uliopangwa, basi viongozi wa mamlaka hiyo hawana sababu ya kuendelea kubaki Bunda, akisisitiza kuwa wananchi wamekuwa wakipata adha kubwa ya kukosa maji.

Sauti ya Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Aswege Enock Kaminyoke

Hatua hiyo ya Mkuu wa Wilaya imekuja ikiwa ni siku moja tangu Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya kuuliza swali la nyongeza Bungeni Dodoma  kuhusu changamoto ya upatikanaji wa maji katika Mji wa Bunda.

Mkurugenzi wa BUWSSA Laurence Misana amewataka wananchi kuwa watulivu, akisema mamlaka hiyo imepokea na kuanza mara moja kutekeleza maagizo ya Mkuu wa Wilaya. Amesema katika kipindi cha saa 24 zilizotolewa, hatua za dharura zimewekwa kuhakikisha wananchi wanaanza kupata maji kama ilivyoelekezwa, huku timu za wataalamu zikiendelea kufanya kazi kurekebisha changamoto zilizopo.

Sauti ya Mkurugenzi wa BUWSSA Laurence Misana