Mazingira FM

Waandishi watakiwa kuelimisha jamii kuhusu ukatili mitandaoni

2 July 2026, 2:40 pm

Mratibu mwandamizi wa program Shirika la C-SEMA Kanda ya Ziwa, Jane David Haule,

Waandishi wa habari wamekuwa na mchango mkubwa katika kupunguza matukio ya ukatili kwenye maeneo mbalimbali

Na Adelinus Banenwa

Imebainika kuwa ukatili unaofanyika kupitia mitandao unaendelea kuongezeka kwa kasi, hali inayoiweka jamii katika hatari zaidi. Kutokana na changamoto hiyo, waandishi wa habari kutoka maeneo mbalimbali nchini wamepatiwa mafunzo ya namna ya kutambua, kuzuia na kuelimisha jamii kuhusu athari za ukatili wa mtandaoni katika warsha iliyofanyika wilayani Tarime, mkoani Mara.

Akizungumza wakati wa warsha hiyo, Mratibu mwandamizi wa program Shirika la C-SEMA Kanda ya Ziwa, Jane David Haule, amesema taasisi hiyo ina imani kuwa kupitia waandishi wa habari kutakuwa na mabadiliko chanya katika jamii kutokana na nafasi kubwa waliyonayo ya kufikisha taarifa kwa wananchi.

Jane David Haule, Mratibu mwandamizi wa program Shirika la C-SEMA Kanda ya Ziwa,

Amesema waandishi wa habari wamekuwa na mchango mkubwa katika kupunguza matukio ya ukatili kwenye maeneo mbalimbali, hivyo wana uwezo pia wa kusaidia kupambana na ukatili wa mtandaoni kwa kuendelea kuelimisha jamii kuhusu madhara yake na namna ya kujikinga.

Sauti ya Jane David Haule

Kwa upande wao, baadhi ya washiriki wa warsha hiyo wamesema mafunzo waliyoyapata yamewaongezea uelewa kuhusu ukatili wa mtandaoni na mbinu za kuuzuia. Wameahidi kutumia taaluma yao kuhakikisha jamii inapata elimu ya kutosha kuhusu athari za ukatili huo pamoja na aina nyingine za ukatili.

Sauti ya baadhi ya washiriki wa warsha hiyo
Baadhi ya washiriki wa warsha hiyo wakiwa katika majadiliano

Naye Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, Siwema Sylvester, amesema serikali kwa kushirikiana na taasisi mbalimbali zisizo za kiserikali, ikiwemo C-SEMA, imeendelea kuchukua hatua za kuelimisha jamii na kutekeleza mikakati mbalimbali ya kutokomeza ukatili wa kijinsia.

Ameongeza kuwa waandishi wa habari ni wadau muhimu katika mapambano hayo na amewataka kuendelea kutumia vyombo vya habari kuelimisha wananchi ili kutokomeza ukatili wa kijinsia, hususan unaowakumba wanawake, watoto na watu wenye ulemavu.

Sauti ya Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Tarime.