Waliojiita wa kisiwani kwa kukosa huduma, sasa wapata maji ya bomba
17 September 2024, 2:29 pm
Upatikanaji wa maji eneo la kisiwani Kilimani kitawezesha wanawake kuepukana na adha ya kuamka asubuh sana na kutembea umbali mrefu kufuata maji.
Na Adelinus Banenwa
Wananchi wa mtaa wa kilimani (kisiwani) kata ya Bunda stoo waishukuru mamlaka ya Maji na usafi wa mazingira Bunda BUWSSA pamoja na diwani wa kata hiyo Flavian Nyamageko kwa kuwasogezea huduma ya maji ya bomba karibu na makazi yao.
Wakazi wa kilimani wameyasema hayo katika uzinduzi wa kituo cha kuchotea maji kwa wakazi wa mtaa huo baada ya mamlaka ya maji Bunda BUWSSA kupitia jitihada za Diwani wa kata hiyo na mwenyekiti wao kuhakikisha maji yanawafikia wakazi waliotaabika kwa muda mrefu.
Akizungumza katika uzinduzi huo mwenyekiti wa mtaa wa Kilimani Ritha Salvatory Ikandiro amesema eneo ambalo leo kituo cha maji kinazinduliwa walijiita kisiwani kutokana na kukosekana kwa huduma muhimu kama vile maji, barabara pamoja na umeme.
Ritha amesema hatua ya kuzindua upatikanaji wa maji litafuta kabisa jina la kisiwani kwa kuwa sasa huduma zote zinakwenda kupatikana katika eneo hilo.
Aidha Ritha amesema uwepo wa kituo cha kuchotea maji karibu na makazi yao kutasaidia wananchi kufanya shughuli zao kwa wakati tofauti na zamani ambapo muda mwingi waliupoteza kwenda kutafuta maji.
Naye mwenyekiti wa mtaa wa idara ya maji Mtaki Bwire amesema jukumu la viongozi ni kushirikiana na wananchi kuhakikisha maendeleo yanapatikana
Mtaki amepongeza jitihada za Diwani wa kata ya Bunda stoo kwa kushirikiana na serikali na wananchi kuhakikisha maendeleo yanapatikana.
Kwa upande wake Diwani wa kata ya Bunda stoo Mhe Flavian Chacha Nyamageko amesema kilio cha huduma ya maji kwa kata ya Bunda stoo kilikuwa kikubwa tangu alipoingia madarakani lakini hadi sasa huduma imesambaa karibu maeneo yote.
Aidha ametoa rai kwa wananchi kuhakikisha wanaitunza miundombinu ya maji hasa mabomba, koki za maji pamoja na kulipa bili za maji ili huduma iweze kuendelea.