Mazingira FM
Mazingira FM
12 December 2025, 8:50 pm

Kwa mwaka mzima tumepata mafanikio mbalimbali ikiwemo kushika nafasi ya pili katika maonesho ya kilimo misitu yaliyoanadaliwa na Vi Agroforestry kutokana na ubora wa bidhaa zinazozalishwa na wakulima wetu.
Na Adelinus Banenwa
Afisa maendeleo wa halmashauri ya mji wa Bunda mkoani Mara Florian Peter amelipongeza shirika la BUFADESO kwa kutekeleza shughuli mbalimbali ambazo zinaleta tija kwa jamii.
Akizungumza katika mkutano mkuu wa shirika hilo uliofanyika leo tarehe 12 Dec 2025 katika ukumbi wa shirika hilo Florian akiwa mgeni rasmi amesema kuna kazi kubwa ambazo BUFADESO wanazifanya ikiwemo kutoa elimu juu ya athari za ukatili wa kijinsia kwenye jamii, elimu wajasiriamali , pamoja na lengo mama la kilimo bora na chenye tija.

Naye afisa maendeleo ya jamii kutoka halmashauri ya wilaya ya Bunda Anneth Laurian amesema ni vema shirika hilo likaendelea kuwa na mshikamano na kuepuka migogoro kwa kuwa kazi wanayoifanya inaonekana na linaisaidia serikali.
Amemtaka mkurugenzi wa shirika la BUFADESO kuwasiliana ana mamlaka za serikali pale wanapokwama katika kuwafikia wananchi walengwa ili waweze kupata msaada pale inapobidi

Naye mkurugenzi wa shirika la BUFADESO Baraka Kamese amesema shirika hilo kwa mwaka mzima wamepata mafanikio mbalimbali ikiwemo kushika nafasi ya pili katika maonesho ya kilimo misitu yaliyoanadaliwa na Vi Agroforestry kutokana na ubora wa bidhaa zinazozalishwa na wakulima wao.
Aidha amewataka wakulima wote katika wilaya za Bunda na Butiama ambao wanatamani kujiunga na BUFADESO wafanye hivyo ili kunufaika na fursa mbalimbali zinazopatikana.