Mazingira FM

Afia nyumba ya kulala wageni akiwa na mpenzi wake

17 May 2026, 9:09 pm

Alisikia sauti ya mwanamke ikiita “Chacha”, “chacha amka umekuwaje huku mtu mwingine akiwa anakoroma”.

Na Adelinus Banenwa

Mwanaume mmoja aliyetambulika kwa jina la Chacha Ryoba (45) mkazi wa Kihumbu kata ya Hunyari halmashauri ya wilaya ya Bunda amepoteza maisha kwenye nyumba ya kulala wageni Bunda akiwa na mpenzi wake.

Tukio hilo linatajwa kutokea May 12 2026 usiku ambapo kwa mujibu wa msimamizi wa nyumba hiyo ya kulala wageni Elizabert Petro aliiambia Mazingira fm kuwa majira ya saa nne aliwapokea wageni hao na wakiwa wanahitaji chumba lakini Chacha alikuwa amelewa na aliwapa kitabu kuandika majina ila walishindwa hivyo alilazimika kuwaandikia kwa kufuata maelezo yao.

Elizabert amesema usiku wakati amelala aliitwa na mlinzi akimtaka Kwenda kukagua chumba kimojawapo kwa kuwa alisikia sauti ya mwanamke ikiita “Chacha”, “chacha amka umekuwaje huku mtu mwingine akiwa anakoroma”.

Elizabert amasema baada ya kufika kwenye kile chumba alimkuta mwanamke nje analia kuomba msaada  na alipoingia ndani ya kile chumba alikuta mwanaume huyo amelala kiubavu ila alionesha kutopumua ndipo alipowaamsha wageni wengine waliomshauri  kuwapigia simu polisi.

Sauti ya Elizabert Petro

Moja wa mashuhuda ambaye ni miongoni mwa wageni kwenye nyumba hiyo Tatu Dira amesema alipoamshwa na msimamizi wa nyumba hiyo na kuona hali ya chumba alishauri asitoke mtu yeyote Kwenye ile nyumba hadi jeshi la polisi lifike kutokana na hali ya mazingira ya marehemu huyo.

Sauti yaTatu Dira

Kwa mujibu Nipashe, upande wake mpenzi wa Chacha Ryoba, amedai kwamba aligundua mabadiliko ya ghafla kwa mwenziwe, baada ya kuanza kuishiwa nguvu na kupata matatizo ya kupumua, kabla ya kufariki dunia muda mfupi baadaye, akiwa katika nyumba ya kulala wageni (guest house), wilayani Bunda, Mkoa wa Mara.

Amesema licha ya juhudi za awali alizozifanya za kujaribu kumsaidia, hali ya Chacha iliendelea kuwa mbaya na baadaye alifariki dunia akiwa ndani ya chumba walichokuwa wamekodi, kwa ajili ya kupumzika.

Jeshi la Polisi Tanzania Mkoa wa Mara, limetoa ufafanuzi kuhusu kifo cha Chacha Ryoba (45) mkulima na mkazi wa Kijiji cha Kihumbu, wilayani Bunda, aliyefariki dunia ghafla, baada ya kudaiwa kupatwa na shambulio la moyo, akiwa na mpenzi wake.

Kwa mujibu wa taarifa ya polisi iliyotolewa leo, tukio hilo lilitokea Mei 12, mwaka huu majira ya saa nne usiku, Chacha aliwasili katika nyumba hiyo ya kulala wageni, akiwa ameongozana na mpenzi wake na kukodi chumba kwa ajili ya kupumzika.