Mazingira FM
Mazingira FM
21 May 2026, 8:27 pm

Baadhi ya miradi imesimama kutokana na changamoto ya upatikanaji wa fedha. Miradi hiyo ni pamoja na mradi wa maji wa Kisangwa, mradi wa ubadilishaji wa mabomba kutoka Migungani kwenda Mlima Kaswaka, pamoja na mradi wa maji taka ambao umefikia asilimia 40.
Na Adelinus Banenwa
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Bunda imeiomba Serikali kutoa fedha kwa ajili ya kukamilisha miradi ya maji inayoendelea kutekelezwa katika mamlaka hiyo huku deni la wateja likifikia milioni 200.
Hayo yameelezwa na mkurugenzi wa mamlaka ya maji bunda BUWSSA Esther Gilyoma alipokuwa akizungumza katika kipindi cha Asubuhi Leo kinachorushwa na Radio Mazingira FM.
Bi. Gilyoma amesema kuwa hali ya upatikanaji na usambazaji wa maji katika mji wa Bunda kwa sasa imefikia asilimia 87, huku miradi mingine ikiendelea kutekelezwa ili kuongeza huduma kwa wananchi.
Ameeleza kuwa baadhi ya miradi imesimama kutokana na changamoto ya upatikanaji wa fedha. Miradi hiyo ni pamoja na mradi wa maji wa Kisangwa, mradi wa ubadilishaji wa mabomba kutoka Migungani kwenda Mlima Kaswaka, pamoja na mradi wa maji taka ambao umefikia asilimia 40 ya utekelezaji wake.
Aidha, Bi. Gilyoma amewataka wananchi kuondoa hofu na kuendelea kuwa na imani na mamlaka hiyo, akisema kuwa mamlaka hiyo inaendelea kufanya kila linalowezekana kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji safi, salama na ya kutosha wakati wote.
Pia ametoa rai kwa wateja wa mamlaka hiyo kuhakikisha wanalipa ankara za maji kwa wakati, ili kuiwezesha mamlaka kuboresha na kuendeleza huduma zake kwa ufanisi zaidi.