Mazingira FM

Wananchi watakiwa kushiri usimamizi wa miradi

29 July 2026, 5:11 pm

Mbunge wa Jimbo la Bunda, Boniphace Getere akiendelea na ziara yake kukagua miradi ya elimu katika jimbo la Bunda 28 July 2026 katika kijiji cha Kurusanga

Hivi karibuni ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Kurusanga utaanza, baada ya kukamilika kwa maandalizi ya awali. Amesema Serikali itatoa shilingi milioni 584 kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo.

Na Mariam Mramba

Mbunge wa Jimbo la Bunda, Boniphace Getere, ametoa wito kwa wananchi wa jimbo hilo kusimamia vizuri miradi ya elimu inayotekelezwa katika maeneo yao ili kuwawezesha watoto kupata elimu bora, akisisitiza kuwa elimu ndiyo urithi muhimu zaidi ambao wazazi wanaweza kuwaachia watoto wao.

Getere ametoa wito huo Julai 28, 2026, alipokuwa akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Kurusanga, Kata ya Salama, katika mwendelezo wa ziara yake ya kikazi ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika jimbo hilo.

Mbunge huyo amesema kuwa hivi karibuni ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Kurusanga utaanza, baada ya kukamilika kwa maandalizi ya awali. Amesema Serikali itatoa shilingi milioni 584 kwa ajili ya ujenzi wa shule hiyo, huku akiwapongeza wananchi wa kijiji hicho kwa jitihada walizoonyesha za kuandaa eneo la mradi na kuweka viashiria vilivyowezesha mradi huo kufikia hatua ya utekelezaji.

Sauti ya Boniphace Getere,

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, George Mbilinyi, Afisa Mazingira wa halmashauri hiyo, Staffa Nashoni, amesema taratibu zote za awali zinazohitajika kwa utekelezaji wa mradi zimekamilika, hivyo ujenzi wa shule hiyo unatarajiwa kuanza wakati wowote.

Wananchi wa Kijiji cha Kurusanga wamempongeza Mbunge Boniphace Getere kwa juhudi zake za kusukuma maendeleo katika jimbo hilo. Pia wamemuomba awasaidie kupata kompyuta kwa ajili ya taasisi zilizopo kijijini hapo ili kurahisisha utendaji wa kazi, wakieleza kuwa kwa sasa huduma nyingi zinaendeshwa kwa kutumia teknolojia.

Sauti za wananchi wa kijiji cha Kurusanga

Katika ziara hiyo, Mbunge Boniphace Getere ametembelea Shule ya Msingi Salama Kati, Shule ya Msingi Masaba, Shule ya Msingi Kurusanga pamoja na eneo litakalojengwa Shule ya Sekondari ya Kurusanga. Aidha, amechangia shilingi milioni 1 kwa ajili ya utengenezaji wa madawati katika Shule ya Msingi Salama Kati.