Mazingira FM
Mazingira FM
27 September 2026, 2:40 pm

“kuna taratibu za kisheria zinazoweza kutumika kuhakikisha mtoto anapata mahitaji yake”
Na Edward Lucas.
Wazazi wametakiwa kutambua kuwa kupata mtoto kunaambatana na wajibu wa kumlea, kumtunza na kumlinda, huku wale wanaoshindwa kutimiza majukumu hayo wakikumbushwa kuwa kuna taratibu za kisheria zinazoweza kutumika kuhakikisha mtoto anapata mahitaji yake.
Kauli hiyo imetolewa na Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Mji wa Bunda, Warioba Juma Warioba, wakati akizungumza katika kipindi cha Mwanga wa Jamii cha Radio Mazingira FM kilichokuwa na mada “Kupata Mtoto ni Uamuzi na Malezi ni Wajibu.”
Warioba amesema changamoto ya mzazi kushindwa kumhudumia mtoto imekuwa miongoni mwa malalamiko yanayofikishwa katika ofisi ya ustawi wa jamii, akisisitiza kuwa wajibu wa malezi unamhusu mzazi, awe mwanamume au mwanamke.
Amesema hali ya kutowajibika kwa mzazi haipaswi kuonekana kama mgogoro wa wazazi pekee, bali inapaswa kuangaliwa kwa kuzingatia maslahi na haki ya mtoto kupata malezi na matunzo, huku akieleza kuwa sheria pia inaweka wajibu kwa baba kutimiza majukumu yake.
Warioba amesema baadhi ya changamoto zinazoweza kujitokeza katika uwajibikaji wa wazazi ni pamoja na kuwepo kwa kauli au mazingira yanayomfanya mzazi mmoja kushindwa kutoa huduma kwa mtoto, akisisitiza kuwa migogoro hiyo inapaswa kushughulikiwa kupitia taratibu zinazotambuliwa kisheria.
Amesisitiza kuwa kupata mtoto ni uamuzi na malezi ni wajibu, hivyo wazazi na walezi wanapaswa kuhakikisha watoto wanapata malezi, matunzo na ulinzi unaostahili, ikiwa ni sehemu ya juhudi za jamii kuzuia ukatili na kutelekezwa kwa watoto.