Mazingira FM

Bunda watakiwa kusalimisha silaha haramu kabla ya Oktoba 31

16 October 2026, 1:27 pm

Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Charles Thobias Mwenya, Mkuu wa Polisi Jamii Wilaya ya Bunda,

Amesisitiza kuwa katika kipindi kilichotengwa kwa ajili ya usalimishaji wa silaha hizo, wananchi wanaozisalimisha hawataulizwa maswali kuhusu silaha wanazokabidhi,

Na Adelinus Banenwa

Jeshi la Polisi Wilaya ya Bunda limewataka wananchi wanaomiliki silaha haramu kuzisalimisha katika vituo vya polisi au ofisi za serikali kabla ya Oktoba 31, 2026, likisisitiza kuwa hatua hiyo inalenga kudhibiti uhalifu na kuimarisha usalama wa wananchi.

Akizungumza kuhusu suala hilo, Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP) Charles Thobias Mwenya, Mkuu wa Polisi Jamii Wilaya ya Bunda, ameeleza kuwa silaha haramu ni pamoja na zile zinazomilikiwa bila kufuata taratibu za kisheria, zikiwemo silaha zinazomilikiwa bila leseni.

Aidha, silaha zinazobaki mikononi mwa watu baada ya wamiliki wake kufariki bila kuripotiwa au kukabidhiwa kwa Jeshi la Polisi, pamoja na silaha zinazotengenezwa kienyeji, zimeainishwa kuwa miongoni mwa silaha zinazopaswa kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria.

Ameongeza kuwa hata silaha inayomilikiwa kihalali inaweza kuhusishwa na uhalifu pale inapotumika kufanya vitendo vya uhalifu.

Sauti ya ASP Charles Thobias Mwenya

Katika wito wake kwa wananchi, ASP Mwenya amewataka wote wenye silaha haramu kuzisalimisha katika vituo vya polisi au ofisi yoyote ya serikali, zikiwemo ofisi za watendaji wa vijiji, mitaa na kata, ili ziweze kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa taratibu zilizowekwa.

Amesisitiza kuwa katika kipindi kilichotengwa kwa ajili ya usalimishaji wa silaha hizo, wananchi wanaozisalimisha hawataulizwa maswali kuhusu silaha wanazokabidhi, kwa mujibu wa utaratibu uliotangazwa.

Hata hivyo, ameeleza kuwa baada ya muda wa usalimishaji kukamilika, operesheni kali zitafanyika kwa lengo la kuwakamata watu wote watakaobainika kumiliki silaha haramu.

Jeshi la Polisi limeweka Oktoba 31, 2026 kuwa siku ya mwisho ya kusalimisha silaha haramu, hivyo wananchi wametakiwa kutumia fursa hiyo kwa hiari kabla ya kuanza kwa operesheni hizo.

Aidha amesema wananchi wametakiwa kushirikiana na Jeshi la Polisi na viongozi wa serikali za mitaa katika kuhakikisha silaha haramu zinaondolewa mikononi mwa watu, hatua inayotarajiwa kusaidia kuzuia uhalifu na kulinda maisha pamoja na mali za wananchi.

Sauti ya ASP Charles Thobias Mwenya