Mazingira FM

Maboto akabidhi miradi ya milion 292 kwa serikali Musoma

28 November 2026, 11:35 am

Amesema mwaka 2016 wananchi walimwomba kuwajengea msingi wa zahanati huku wao wakiahidi kukamilisha ujenzi, lakini kwa kipindi cha miaka 10 mpango huo haukufanikiwa.

N Adelinus Banenwa

Mkurugenzi wa Maboto Microfinance, Robert Maboto, amekabidhi kwa Serikali miradi miwili ya kijamii yenye thamani ya jumla ya shilingi milioni 292, ikiwemo zahanati ya Kijiji cha Muhoji iliyogharimu shilingi milioni 250 na nyumba ya walimu katika Shule ya Msingi Muhoji iliyojengwa kwa shilingi milioni 42, kwa lengo la kuboresha huduma za afya na elimu kwa wananchi.

Akikabidhi zahanati hiyo, Maboto amesema ameamua kuwekeza katika ujenzi wa kituo hicho ili kuwaondolea wananchi adha ya kutembea umbali wa takribani kilometa 20 kwenda na kurudi kutafuta huduma za afya, hali iliyokuwa ikiwaathiri zaidi wanawake wajawazito.

Mkurugenzi wa Maboto Microfinance, Robert Maboto

Amesema mwaka 2016 wananchi walimwomba kuwajengea msingi wa zahanati huku wao wakiahidi kukamilisha ujenzi, lakini kwa kipindi cha miaka 10 mpango huo haukufanikiwa. Hali hiyo ilimfanya kuamua kuanza ujenzi mwezi Juni mwaka huu, ambao umekamilika ndani ya miezi minne. Sambamba na hilo, amekabidhi nyumba ya walimu yenye uwezo wa kuishi familia mbili.

Sauti ya Robert Maboto
baadhi ya viongozi kweye picha ya pamoja wakati Maboto akikabidhi jengo la zahanati kijiji cha Muhoji

Akizungumza wakati wa kupokea na kuzindua majengo hayo, Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Mhe. Juma Chikoka, amempongeza Maboto kwa mchango wake katika kuboresha huduma za kijamii, huku akiwataka wananchi kutunza miundombinu hiyo ili iweze kudumu. Pia amewataka watumishi watakaopangiwa kufanya kazi katika zahanati hiyo kuishi ndani ya kijiji hicho ili waweze kutoa huduma kwa wakati, akisisitiza maelekezo hayo kwa watumishi wote wa Halmashauri ya Wilaya ya Musoma. Aidha, amewahimiza wanawake wajawazito kuhudhuria kliniki kwa wakati.

Sauti ya Mhe. Juma Chikoka
Jengo sehemu ya nyuma lililokabidhiwa kwa serikali baada ya kujengwa na mdau wa maendeleo Robert Maboto lililoghrarimu milioni 250.5
Jengo sehemu ya mbele lililokabidhiwa kwa serikali baada ya kujengwa na mdau wa maendeleo Robert Maboto lililoghrarimu milioni 250.5

Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Muhoji wamemshukuru Maboto kwa kuwajengea zahanati hiyo, wakieleza kuwa awali walilazimika kufuata huduma za afya Masinono au Bunda. Wamesema hali ilikuwa ngumu zaidi wakati wa mvua, huku wanawake waliopata uchungu nyakati za usiku wakikabiliwa na changamoto ya kufika hospitalini na wakati mwingine kujifungulia njiani. Wameongeza kuwa walikuwa wakitumia zaidi ya shilingi elfu 20 kwa ajili ya usafiri wa kwenda kupata huduma za afya.

Sauti za baadhi ya wananchi