Mazingira FM
Mazingira FM
19 October 2026, 6:01 pm

Kongamano la 11 la Kilimo na Misitu lililodhaminiwa na Shirika la Vi Agroforestry na kufanyika Bweri, wilayani Musoma, ambapo amesisitiza umuhimu wa kuwaandalia vijana mazingira yatakayowawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji.
Na Adelinus Banenwa
Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Gerard Kusaya, amezitaka halmashauri zote mkoani humo pamoja na taasisi za kifedha kuandaa programu maalumu za kuwawezesha vijana kushiriki katika mnyororo wa thamani wa kilimo na misitu, ili waweze kutumia fursa zilizopo katika sekta hizo kujikwamua kiuchumi.
Kusaya ametoa wito huo wakati wa ufunguzi wa Kongamano la 11 la Kilimo na Misitu lililodhaminiwa na Shirika la Vi Agroforestry na kufanyika Bweri, wilayani Musoma, ambapo amesisitiza umuhimu wa kuwaandalia vijana mazingira yatakayowawezesha kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji na biashara.
Amesema mnyororo wa thamani katika kilimo na misitu una fursa nyingi za kiuchumi ambazo vijana wanaweza kuzitumia kujipatia kipato na kujiajiri, ikiwemo uzalishaji wa mbegu bora, ufugaji wa nyuki na usindikaji wa matunda. Hata hivyo, amesema ili vijana wanufaike na fursa hizo, wanahitaji kuwezeshwa kupitia programu zinazowaunganisha na rasilimali fedha pamoja na elimu ya biashara.

Kwa upande wake, Stellah Msami kutoka Shirika la Vi Agroforestry amesema maonesho ya mwaka huu yamelenga kutoa elimu kwa vijana kuhusu namna wanavyoweza kushiriki na kunufaika na mnyororo wa thamani katika kilimo na misitu.
Msami amesema kupitia kongamano hilo, vijana wanapata fursa ya kujifunza shughuli mbalimbali za kiuchumi zinazohusiana na kilimo na misitu, hatua inayolenga kuwajengea uwezo wa kutumia fursa zilizopo kujiajiri, kuongeza kipato na kuchangia maendeleo ya jamii zao.