Mazingira FM
Mazingira FM
6 October 2026, 8:29 pm

Inadaiwa kuwa mtuhumiwa alimpiga Magreth kichwani kwa kutumia kitu butu, kabla ya kumchoma sehemu mbalimbali za mwili kwa kitu chenye ncha kali.
Na Adelinus Banenwa
Mwanasheria Keneth Nkiko (28) anashikiliwa na Polisi Mkoa wa Mara kwa tuhuma za kumuua Magreth Richard (22), mfanyabiashara na mkazi wa Mtaa wa Mwigobero, Manispaa ya Musoma.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Pius Lutumo, tukio hilo limetokea Jumatatu, Oktoba 5, 2026, majira ya saa nne asubuhi, huku polisi wakiendelea na uchunguzi kubaini mazingira ya tukio hilo.
Kamanda Lutumo amesema Nkiko, ambaye alikuwa akitoa msaada wa kisheria kwa waathirika wa vitendo vya ukatili wa kijinsia, anadaiwa kumuua Magreth ambaye alikuwa mpenzi wake.
Inadaiwa kuwa mtuhumiwa alimpiga Magreth kichwani kwa kutumia kitu butu, kabla ya kumchoma sehemu mbalimbali za mwili kwa kitu chenye ncha kali. Magreth alipatwa na majeraha makubwa yaliyosababisha kupoteza damu nyingi na kufariki dunia.
Uchunguzi wa awali wa polisi unaonyesha kuwa chanzo kinachodaiwa kuhusishwa na tukio hilo ni wivu wa kimapenzi, ambapo Nkiko alikuwa akimtuhumu mpenzi wake kuwa na mahusiano na wanaume wengine.
Polisi wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.