Mazingira FM
Mazingira FM
24 October 2026, 7:44 pm

Mbunge huyo ameeleza kuwa ataendelea kupigania suala la kikokotoo pamoja na changamoto zinazohusu Bodi ya Walimu,
Na Adelinus Banenwa
Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini, Mhe. Esther Bulaya, amesema ataendelea kupigania maslahi ya walimu na watumishi wengine wa umma, akiahidi kuendelea kuibua bungeni changamoto zinazowakabili, ikiwemo suala la kikokotoo na Bodi ya Walimu.
Bulaya amesema hatakubali walimu kuendelea kukabiliwa na bughudha katika utekelezaji wa majukumu yao, akisisitiza kuwa ataendelea kuwasemea na kutetea maslahi yao ili wafanye kazi katika mazingira yenye amani na utulivu.

Amesema hayo leo, Oktoba 24, 2026, wakati wa maadhimisho ya Siku ya Walimu yaliyofanyika wilayani Bunda, mkoani Mara, ambapo amesisitiza dhamira yake ya kuendelea kufuatilia changamoto za walimu kupitia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Mbunge huyo ameeleza kuwa ataendelea kupigania suala la kikokotoo pamoja na changamoto zinazohusu Bodi ya Walimu, akiahidi kuziwasilisha na kuzisemea bungeni ili zipatiwe ufumbuzi.

Aidha, katika maadhimisho hayo, Mhe. Esther Bulaya ametoa motisha yenye thamani ya shilingi milioni 17 kwa walimu na shule zilizofanya vizuri katika Jimbo la Bunda Mjini. Motisha hiyo imejumuisha fedha taslimu na makombe kwa shule zilizofanya vizuri, pamoja na fedha taslimu na vyeti kwa walimu waliofanya vizuri, ikiwa ni sehemu ya kutambua juhudi na mchango wao katika kuboresha sekta ya elimu na kuwahamasisha kuendelea kuongeza bidii katika ufundishaji ili kuinua kiwango cha ufaulu kwa wanafunzi.
Awali, Mwalimu Andrew Nyawena, mjumbe wa Kamati Tendaji ya Chama cha Walimu Tanzania (CWT), amemuomba Bulaya kuendelea kulifanyia kazi suala la kikokotoo, akieleza kuwa limekuwa miongoni mwa ajenda muhimu zinazohitaji kufuatiliwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Aidha, Nyawena ameeleza kuwa kuna changamoto zinazohitaji kuangaliwa katika taratibu za Bodi ya Walimu, hususan kuhusu upatikanaji wa leseni za ualimu.

Amehoji utaratibu unaomtaka mwalimu kwenda kusoma ili kupata leseni, akitaka kujua ni nani atakayebaki shuleni kufundisha wanafunzi wakati walimu wanapokuwa wameondoka kuhudhuria masomo hayo.
Nyawena amesisitiza umuhimu wa kuzingatia mazingira halisi ya kazi za walimu katika kuweka taratibu za kitaaluma, ili kuhakikisha walimu wanaendelea kutekeleza majukumu yao huku changamoto zao zikishughulikiwa.