Mazingira FM
Mazingira FM
1 October 2026, 2:06 pm

Wazee wana nafasi kubwa katika jamii kutokana na uzoefu, hekima na mchango wao katika malezi, maendeleo na ujenzi wa taifa.
Na Adelinus Banenwa
Maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani, ambayo huadhimishwa kila mwaka Oktoba Mosi, yamekuwa fursa kwa wazee wa Baraza la Wazee Wilaya ya Bunda kueleza changamoto zinazowakabili katika jamii, zikiwemo kauli za baadhi ya vijana wanaodai kuwa wazee wamepitwa na wakati.
Wakizungumza na Radio Mazingira FM katika mahojiano maalumu yaliyofanyika kuelekea maadhimisho hayo, wazee hao wamesema wanakerwa na kauli hizo, wakieleza kuwa wazee wana nafasi kubwa katika jamii kutokana na uzoefu, hekima na mchango wao katika malezi, maendeleo na ujenzi wa taifa. Wamewataka vijana kuwaheshimu wazee na kuthamini mchango wao katika jamii badala ya kuwadharau kwa kigezo cha umri.
Aidha, wazee hao wameiomba serikali kuboresha huduma za afya kwa wazee ili waweze kupata matibabu kwa urahisi na kwa wakati. Wamesisitiza umuhimu wa kuboresha utaratibu wa utoaji wa huduma za afya kwa kutumia vitambulisho vya wazee, ili kuondoa usumbufu wanaokutana nao wanapohitaji matibabu. Wameeleza kuwa hatua hiyo itasaidia kulinda afya zao na kuhakikisha wanapata huduma zinazostahili katika kipindi hiki cha uzee.