Mazingira FM

Mtoto wa miaka 12 adaiwa kulawitiwa Bunda

29 October 2026, 9:20 pm

muhanga wa tukio

Baba mzazi wa mtoto huyo ameiomba Serikali kumsaidia mwanawe kupata mazingira salama ya kuishi, akieleza kuwa mtoto anakabiliwa na aibu na fedheha kutokana na tukio hilo

Na Adelinus Banenwa

Mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka 12, mkazi wa Kijiji cha Bulamba, Kata ya Butimba, Halmashauri ya Wilaya ya Bunda, mkoani Mara, anadaiwa kufanyiwa ukatili wa kingono akiwa machungani. Tukio hilo linadaiwa kutokea Oktoba 3, 2026, majira ya mchana, wakati mtoto huyo akichunga mifugo pamoja na wenzake.

Kwa mujibu wa watoto hao mtuhumiwa alidai kuwa mtoto huyo na wenzake walikuwa wakilisha mifugo katika shamba lake, madai ambayo yamekanushwa na mtoto huyo pamoja na wenzake.

Akizungumza na Radio Mazingira FM, mtoto huyo amedai kuwa mtuhumiwa aliwafukuza wenzake waliokuwa wakichunga naye, kisha akamvuta mtoto huyo hadi kwenye korongo ambako anadaiwa kumfanyia ukatili huo.

Sauti ya muhanga wa tukio la ukatili

Kwa upande wake, mmoja wa watoto waliokuwa machungani pamoja na mhanga amesema kuwa mtuhumiwa aliwatishia kuwadhuru iwapo wangesogea eneo alilokuwa. Amesema hali hiyo ilimfanya akimbie nyumbani ili kutoa taarifa kuhusu mwenzake, ambaye alidai kuwa amechukuliwa na mtu huyo.

Sauti ya shuhuda
Sauti ya Baba mzazi wa muhanga

Baba mzazi wa mtoto huyo ameiomba Serikali kumsaidia mwanawe kupata mazingira salama ya kuishi, akieleza kuwa mtoto anakabiliwa na aibu na fedheha kutokana na tukio hilo. Aidha, ameiomba Serikali kuchukua hatua dhidi ya wanaotenda vitendo vya ukatili ili kuzuia matukio kama hayo katika jamii.

Sauti ya Baba mzazi wa muhanga

Kwa upande wake, Afisa Ustawi wa Jamii wa kata ya Butimba, Halmashauri ya Wilaya ya Bunda,Evona Alphonce Norasco amethibitisha kuwa taarifa ya tukio hilo ipo na kwamba shauri hilo linaendelea mahakamani. Amesema mtuhumiwa anatarajiwa kufikishwa mahakamani Novemba 2, 2026, kwa ajili ya kutajwa kwa kesi hiyo, huku akitoa wito kwa jamii kulinda watoto na kutoa taarifa kwa mamlaka husika pale wanapobaini vitendo vya ukatili dhidi yao.

Sauti ya Evona Alphonce Norasco