Mazingira FM
Mazingira FM
9 October 2026, 3:03 pm

Mbali na fedha hizo, Bulaya ameahidi kuchangia matofali 2,500, kuweka umeme katika vyumba vitano vya madarasa
Na Taro Michael Mujora
Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini, Esta Bulaya, achangia shilingi milioni tano kwa ajili ya maendeleo ya Shule ya Sekondari Nyiendo, kupitia mwakilishi wake, Dr Wilson Mukama, katika mahafali ya 19 ya Kidato cha Nne ya shule hiyo.
Kati ya fedha hizo, shilingi milioni nne tayari zimetolewa, huku milioni moja iliyobaki akiahidi kuikamilisha, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha mazingira ya ufundishaji na ujifunzaji.
Mbali na fedha hizo, Bulaya ameahidi kuchangia matofali 2,500, kuweka umeme katika vyumba vitano vya madarasa na kugharamia masomo ya wanafunzi wanne katika vyuo vya ndani ya nchi.
Katika mpango huo wa ufadhili wa masomo, wanafunzi watatu, wakiwemo wasichana wawili na mvulana mmoja, watasomea Uhandisi Bahari, huku mwanafunzi mwingine wa kiume akisomea Sayansi ya Udongo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari Nyiendo, Mwalimu Neema Peter Charles, ameeleza kuwa shule hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali zinazohitaji ushirikiano wa wadau, zikiwemo upungufu wa kompyuta za mezani 10, ukosefu wa jiko la kupikia na baadhi ya madarasa kutokuwa na umeme.

Awali, wanafunzi katika risala yao walitaja changamoto nyingine kuwa ni upungufu wa walimu wa masomo ya Sayansi na Hisabati, ukosefu wa hosteli kwa wasichana, uhaba wa vitabu vya kujisomea, changamoto za upatikanaji wa chakula pamoja na uhaba wa nyumba za walimu.
Mahafali hayo yamehitimisha safari ya wanafunzi 236 wa Kidato cha Nne, wakiwemo wavulana 117 na wasichana 119.