Mazingira FM
Mazingira FM
2 October 2026, 6:31 am

Shule hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo ukosefu wa jiko la kupikia chakula, uzio wa shule pamoja na baadhi ya wazazi kutoshiriki kikamilifu katika kuchangia chakula cha wanafunzi
Na Adelinus Banenwa
Shule ya Sekondari Kabasa wilayani Bunda mkoani Mara imefanikiwa kupata zaidi ya shilingi milioni 14 kwa ajili ya ujenzi wa jiko la kupikia chakula cha wanafunzi.
Jumla ya shilingi milioni 14. zimepatikana katika mahafali ya 20 ya kidato cha nne ya shule hiyo, ambapo wanafunzi 137 wanatarajiwa kufanya mtihani wa kuhitimu kidato cha nne mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa ya shule iliyosomwa na Mkuu wa Shule, Godfrey Maiga Maduhu, pamoja na risala ya wanafunzi, shule hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo ukosefu wa jiko la kupikia chakula, uzio wa shule pamoja na baadhi ya wazazi kutoshiriki kikamilifu katika kuchangia chakula cha wanafunzi.

Katika hatua ya kukabiliana na changamoto hiyo, mgeni rasmi katika mahafali hayo, Yusuph Jackson Nyanya, kwa kushirikiana na wageni wengine waalikwa, akiwemo Mbunge wa Bunda Mjini, Esther Bulaya, wamechangia kiasi cha shilingi milioni 13.3 kwa ajili ya ujenzi wa jiko hilo, huku zaidi ya shilingi milioni moja ikiwa imeahidiwa.
Akizungumza baada ya kutangazwa kwa kiasi cha fedha kilichopatikana, Diwani wa Kata ya Kabasa, Daniel Yona Magembe, amesema fedha hizo zitasimamiwa kwa umakini ili kuhakikisha zinatumika kutekeleza lengo lililokusudiwa.