Mazingira FM
Mazingira FM
6 October 2026, 1:27 pm

Aswege amemuomba Mkuu wa Wilaya mpya kuendelea kushirikiana na wananchi wa Bunda, akieleza kuwa wananchi hao ni wakarimu na wana ushirikiano
Na Adelinus Banenwa
Aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Aswege Enock Kaminyoge, amekabidhi ofisi kwa Mkuu mpya wa Wilaya hiyo, Dkt. Khalfani Haule, katika hafla iliyofanyika Oktoba 5, 2026 katika ofisi za Mkuu wa Wilaya ya Bunda.
Akizungumza katika makabidhiano hayo, Kaminyoge ameishukuru Serikali kwa kuendelea kumuamini na kumpa nafasi ya kuhudumu kwa miaka miwili zaidi baada ya kutimiza umri wa kustaafu utumishi wa umma.
Aidha, amemuomba Mkuu wa Wilaya mpya kuendelea kushirikiana na wananchi wa Bunda, akieleza kuwa wananchi hao ni wakarimu na wana ushirikiano.
Kwa upande wake, Dkt. Haule amemshukuru Rais kwa kuendelea kumuamini na kumteua kuwa Mkuu wa Wilaya, huku akiwaomba watumishi wa halmashauri, wakiwemo wakurugenzi, kuhakikisha miradi inatekelezwa kwa mujibu wa taratibu.
Makabidhiano hayo yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali, wakiwemo wajumbe wa Kamati ya Usalama ya Wilaya, wakurugenzi wa halmashauri zote mbili, wakuu wa taasisi pamoja na viongozi wengine.