Mazingira FM
Mazingira FM
10 November 2026, 7:21 am

Hii ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha mazingira ya upishi na utoaji wa huduma ya chakula kwa wanafunzi.
Na Adelinus Banenwa
Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini, Mhe. Ester Amos Bulaya, ametimiza ahadi yake kwa kukabidhi jiko la kisasa la kupikia lenye thamani ya Shilingi milioni 2.5 kwa Shule ya Sekondari Sizaki.
Hii ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuboresha mazingira ya upishi na utoaji wa huduma ya chakula kwa wanafunzi.

Jiko hilo limekabidhiwa na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Bunda, Mhe. Lucas Daniel Marco, kwa niaba ya Mbunge huyo, ambaye amesema kuwa baada ya kuona umuhimu wa msaada huo, amepokea ombi jingine la shule hiyo la kuhitaji jiko la ziada ili kuondoa kabisa changamoto ya upishi wa chakula kwa wanafunzi.

Mhe. Marco amesema atahakikisha ombi hilo linafikishwa kwa Mhe. Bulaya ili liweze kufanyiwa kazi, akieleza kuwa ni muhimu shule hiyo kuwa na mazingira bora ya kuandaa chakula kwa wanafunzi.
Kwa upande wake, Katibu wa Siasa na Uenezi wa CCM Wilaya ya Bunda, Ndugu Gasper Charles, amempongeza Mhe. Bulaya kwa kutekeleza ahadi hiyo aliyotoa Oktoba 7, 2026, wakati wa mahafali ya Kidato cha Nne katika shule hiyo.

Viongozi hao pia wametoa wito kwa uongozi wa shule na jamii kwa ujumla kuhakikisha jiko hilo linatunzwa vizuri ili liweze kudumu na kuendelea kutoa huduma kwa muda mrefu.

walimu na wanafunzi, wameishukuru Mbunge huyo kwa msaada huo, wakieleza kuwa jiko hilo litasaidia kuboresha mazingira ya maandalizi ya chakula na kurahisisha upishi kwa ajili ya wanafunzi.