Mazingira FM

Usaliti na kutokuaminiana vyatajwa kuchangia ukatili kwenye ndoa

25 November 2026, 9:42 am

Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Mji wa Bunda, Warioba Juma Warioba

Baadhi ya wanandoa wamekuwa wakifanya maamuzi kuhusu mali na uwekezaji bila kuwashirikisha wenza wao, jambo linaloweza kuibua kutokuelewana na migogoro ndani ya familia.

Na Adelinus Banenwa

Kutoaminiana baina ya wanandoa kumetajwa kuwa miongoni mwa sababu zinazochangia kufichana kwa taarifa za umiliki wa mali katika ndoa, hali inayoweza kusababisha migogoro na kuchochea vitendo vya ukatili katika jamii.

Hali hiyo inadaiwa kuchangiwa na changamoto mbalimbali ikiwemo usaliti katika ndoa, ukosefu wa uaminifu na baadhi ya wanandoa kujenga au kuwekeza mali katika familia zao bila kuwashirikisha wenza wao.

Akizungumzia suala hilo, Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Mji wa Bunda, Warioba Juma Warioba, amesema kutoaminiana kunapokosekana uwazi katika masuala ya umiliki wa mali, huweza kuongeza migogoro baina ya wanandoa.

Amesema baadhi ya wanandoa wamekuwa wakifanya maamuzi kuhusu mali na uwekezaji bila kuwashirikisha wenza wao, jambo linaloweza kuibua kutokuelewana na migogoro ndani ya familia.

Warioba ameyasema hayo wakati akizungumzia kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia, akisisitiza umuhimu wa wanandoa kujenga uaminifu, uwazi na kushirikishana katika masuala ya umiliki na usimamizi wa mali ili kuimarisha mahusiano ya kifamilia na kupunguza migogoro inayoweza kusababisha ukatili katika jamii.

Sauti ya Afisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Mji wa Bunda, Warioba Juma Warioba