Mazingira FM
Mazingira FM
23 October 2026, 4:42 pm

Mtambi amemuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara pamoja na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Tarime Rorya kuhakikisha madereva wote wa bodaboda watakaobainika kukiuka sheria hizo wanakamatwa
Na Adelinus Banenwa
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Brigedia Jenerali Evance Alfred Mtambi, ametoa onyo kali kwa madereva wa bodaboda wanaokiuka sheria za usalama barabarani, akipiga marufuku vitendo vya kuendesha kwa mwendo kasi, kutumia gurudumu moja na kukata mfumo wa kutolea moshi (exhaust) ili pikipiki kutoa mlio mkali.
Mtambi amemuagiza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara pamoja na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kipolisi Tarime Rorya kuhakikisha madereva wote wa bodaboda watakaobainika kukiuka sheria hizo wanakamatwa na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Amesisitiza kuwa madereva wa bodaboda wanapaswa kuzingatia sheria za usalama barabarani na kuacha vitendo vinavyoweza kuhatarisha maisha yao, abiria pamoja na watumiaji wengine wa barabara.

Katika hatua nyingine, Mtambi amewaagiza wakuu wote wa wilaya za Mkoa wa Mara kuhakikisha madereva wa bodaboda wanakuwa na vyeti vya mafunzo ya udereva pamoja na leseni halali za kuendesha pikipiki.
Aidha, amewataka wakuu hao wa wilaya kusimamia kikamilifu utekelezaji wa agizo hilo ili kuhakikisha madereva wanaotoa huduma za usafiri wa abiria kwa pikipiki wanakidhi masharti ya udereva na kuzingatia taratibu zilizowekwa.
Brigedia Jenerali Mtambi ametoa maelekezo hayo wakati wa ufunguzi wa awamu ya pili ya mpango wa Bima ya Afya kwa Wote, uliofanyika katika viwanja vya Shule ya Msingi Mkendo, wilayani Musoma, mkoani Mara.