Mazingira FM
Mazingira FM
9 October 2026, 9:50 am

Amesema vitisho vya kiusalama vilivyokuwa vikijitokeza hapo awali viliwafanya baadhi ya wawekezaji kuhofia kuwekeza mkoani Mara.
Na Adelinus Banenwa
Mkuu wa Mkoa wa Mara, Brigedia Jenerali Evance Alfred Mtambi, ametoa onyo kali kwa watu wanaohatarisha usalama wa mkoa huo, akisisitiza kuwa watachukuliwa hatua haraka bila kujali mazingira, iwe mvua au jua.
Brigedia Jenerali Mtambi ametoa kauli hiyo wakati wa kikao cha wadau wa kujadili maendeleo ya Mkoa wa Mara kilichofanyika Wilaya ya Tarime, akitumia kauli “atakaye na aje” kusisitiza msimamo wake dhidi ya watu wanaovuruga amani na usalama.
Amesema vitisho vya kiusalama vilivyokuwa vikijitokeza hapo awali viliwafanya baadhi ya wawekezaji kuhofia kuwekeza mkoani Mara, hali inayoweza kuathiri fursa za kiuchumi na maendeleo ya wananchi.
Kutokana na hali hiyo, amewahimiza wawekezaji wenye nia ya kuwekeza mkoani humo kujitokeza na kutumia fursa zilizopo, akieleza kuwa Mkoa wa Mara una fursa nyingi za uwekezaji na kwamba usalama ni wa uhakika.
Aidha, RC Mtambi amesema kuwa kwa mujibu wa takwimu za Wizara ya Mambo ya Ndani alizorejelea, Mkoa wa Mara haupo miongoni mwa mikoa 15 inayotajwa kuwa na changamoto za kiusalama, na hata orodha inapofikia mikoa 20, mkoa huo bado haujajumuishwa.
Amesisitiza kuwa kuimarika kwa usalama ni muhimu katika kuvutia wawekezaji, kukuza uchumi na kuharakisha maendeleo ya Mkoa wa Mara.