Mazingira FM

Wasira: “Amani ndiyo msingi wa maendeleo ilindeni”

13 October 2026, 11:36 am

Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Kambarage Wasira

“Tusichezee amani kwa kuwa msingi wa maendeleo ni uwepo wa amani thabiti na tanazania tumepewa amani hiyo”

Na Adelinus Banenwa

Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Kambarage Wasira, amewataka Watanzania kudumisha amani nchini, akisisitiza kuwa amani ni msingi muhimu wa maendeleo katika jamii.

Wasira ameyasema hayo wakati akizungumza na wakazi wa Bunda, mkoani Mara, alipofika kuwasalimia. Amesema tangu achaguliwe kuwa mbunge wa Afrika Mashariki, amezidi kutambua umuhimu wa amani katika kuimarisha maendeleo na ustawi wa wananchi.

Akifafanua umuhimu wa amani, Wasira ametolea mfano wa mkutano wa hivi karibuni uliofanyika nchini Somalia, ambao ulifanyika katika uwanja wa ndege kutokana na wasiwasi wa kiusalama.

Amesema hali hiyo ni kielelezo cha changamoto zinazoweza kujitokeza pale ambapo masuala ya usalama yanapokuwa na mashaka, hivyo kuwataka Watanzania kuendelea kuthamini, kulinda na kudumisha amani ili kuweka mazingira bora kwa maendeleo ya taifa.

Aidha, Wasira amesisitiza kuwa amani ni jukumu la kila Mtanzania bila kujali tofauti za kisiasa, kijamii au kiitikadi. Amesema wananchi wanapaswa kuendelea kushirikiana, kuheshimiana na kutatua tofauti zao kwa njia ya mazungumzo ili kuepusha migogoro inayoweza kuhatarisha utulivu na mshikamano katika jamii.

Ameongeza kuwa ni muhimu kwa wananchi kutambua thamani ya amani na kuilinda kwa vitendo, kwani mazingira yenye utulivu huwezesha shughuli za kiuchumi na kijamii kufanyika kwa ufanisi.

Hivyo, amewahimiza wakazi wa Bunda na Watanzania kwa ujumla kuwa mabalozi wa amani katika maeneo yao, kwa lengo la kuhakikisha nchi inaendelea kuwa salama na wananchi wanapata fursa ya kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.

Sauti ya Kambarage Wasira