Mazingira FM
Mazingira FM
1 November 2026, 1:12 pm

Katika kipindi ambacho vijana wengi wanakabiliwa na changamoto ya ajira na mitaji mfanyabiashara wa dawa za kudhibiti wadudu, anatoa somo kuwa biashara inaweza kuanza kwa mtaji mdogo.
Na Catherine Msafiri,
Katika kipindi ambacho vijana wengi wanakabiliwa na changamoto ya ajira na mitaji ya kuanzisha biashara, simulizi ya Lwige Mayala, mfanyabiashara wa dawa za kudhibiti wadudu, inatoa somo kuwa biashara inaweza kuanza kwa mtaji mdogo.
Lwige, anayefanyia biashara katika mtaa wa Saranga, Bunda, anasema safari yake ya kibiashara ilianza kwa mtaji wa shilingi elfu hamsini.
Kwa vijana wengi, ndoto ya kujiajiri wakati mwingine hukwama kutokana na dhana kuwa biashara inahitaji mtaji mkubwa ili kuanza.
Hata hivyo, Lwige Mayala, muuza dawa za kudhibiti wadudu wakiwemo mende, kunguni, panya na viroboto, ni miongoni mwa wafanyabiashara wanaoonyesha umuhimu wa kuanza na kile kilichopo.
Kupitia biashara yake katika Mtaa wa Saranga, Bunda, Lwige anaweka mfano wa namna mtaji mdogo unavyoweza kuwa hatua ya kwanza katika kujenga shughuli ya kujipatia kipato.

Lwige anadhihirisha wazi ule msemo wa wahenga kwamba kufeli masomo sio kufeli maisha huku akieleza kuwa baada ya kuhitimu darasa la saba na matokeo hayakua mazuri bado aliamini akiwekeza nguvu kwenye biashara atafanikiwa.
Pia akilenga yeye kama kijana kujiepusha na ujana na kupindukia kwenye makundi.
Uzoefu huu unatoa ujumbe kwa vijana kuwa kuanzisha biashara kunahitaji zaidi ya mtaji pekee. Ni muhimu pia kutambua mahitaji ya wateja, kupanga matumizi, kuweka kumbukumbu za mauzo na faida, pamoja na kuzingatia sheria na usalama wa bidhaa zinazouzwa.
Kwa biashara ya dawa za kudhibiti wadudu, uuzaji na matumizi salama ya bidhaa hizo ni jambo la msingi, kwa kuzingatia maelekezo ya matumizi na tahadhari zinazotolewa na mtengenezaji.