Mazingira FM
Mazingira FM
7 November 2026, 1:57 pm

Viongozi, wazazi na jamii kwa ujumla watakiwa kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya ukeketaji, kuhakikisha kuwa vitendo hivyo havipaswi kuvumiliwa.
Na Edward Lucas.
Serikali ya Halmashauri ya Wilaya ya Rorya mkoani Mara imezindua kampeni maalumu ya kupinga vitendo vya ukeketaji, ikiwa na lengo la kulinda haki, afya na usalama wa mtoto wa kike.
Kampeni hiyo iliyoanzishwa na kuratibiwa na Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, inalenga kuongeza uelewa kwa jamii kuhusu madhara ya ukeketaji, kuimarisha mifumo ya ulinzi wa mtoto wa kike pamoja na kuhakikisha mila na desturi zinazohatarisha maisha na ustawi wa watoto zinaachwa.
Akizungumza katika uzinduzi wa kampeni hiyo uliofanyika tarehe 6 Novemba 2026 katika viwanja vya Shule ya Sekondari ya Kisumwa, Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Stanslaus Mabula, amewataka viongozi, wazazi na jamii kwa ujumla kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi ya ukeketaji, akisisitiza kuwa vitendo hivyo havipaswi kuvumiliwa.
Kwa upande wake, Mratibu wa Dawati la Kitaifa la Kutokomeza Vitendo vya Ukeketaji kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, amesema mkakati ulioandaliwa na wizara kwa kushirikiana na wadau mbalimbali unalenga kupunguza kiwango cha ukeketaji nchini kutoka asilimia nane ya sasa hadi asilimia nne ifikapo mwaka 2029/2030.
Amesema kufikiwa kwa lengo hilo kunahitaji ushirikiano wa karibu kati ya serikali, viongozi wa kimila, wazazi na jamii kwa ujumla ili kuhakikisha mtoto wa kike analindwa dhidi ya vitendo hivyo vinavyokiuka haki zake.
