Mazingira FM

Mwili wa mwanamke wakutwa umetelekezwa kwenye pagale

6 July 2026, 1:25 pm

Jengo ambalo mwili ulikutwa

Baadhi ya wananchi wameeleza kuwa walikuwa wakimuona marehemu mara kwa mara katika eneo hilo, ingawa hawakufahamu alikotoka

Na Edward Lucas

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara limethibitisha kuokotwa kwa mwili wa mwanamke ndani ya jengo lililotelekezwa la Wasira, lililopo eneo la Manyamanyama katika Halmashauri ya Mji wa Bunda mkoani Mara.

Mwili huo uligunduliwa na wananchi jumamosi tarehe 4 July 2026 majira ya saa 3:00 Asubuhi kufuatilia harufu kali iliyokuwa ikitoka ndani ya jengo hilo kwa siku kadhaa na kutoa taarifa kwa viongozi wa eneo husika.

Sauti ya Rhoda

Mjumbe wa Serikali ya Mtaa wa Mbugani, Kata ya Manyamanyama, Yohana Josia maarufu Manumbu wa Manumbu, amesema baada ya kupokea taarifa hizo, viongozi wa eneo kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi walifika eneo la tukio na kuuchukua mwili kwa ajili ya uchunguzi pamoja na utambuzi.

Sauti ya Yohana Josia

Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara, Pius Lutumo amesema baadhi ya wananchi wameeleza kuwa walikuwa wakimuona marehemu mara kwa mara katika eneo hilo, ingawa hawakufahamu alikotoka, huku akionekana kuishi katika mazingira magumu au kuwa na changamoto ya afya ya akili.

Kamanda amesema uchunguzi wa awali unaonesha kuwa huenda kifo hicho kilitokana na sababu za kawaida, huku mwili ukiendelea kuhifadhiwa katika Kituo cha Afya Bunda kwa ajili ya utambuzi. Aidha, ametoa wito kwa wananchi wenye ndugu aliyepotea kufika kituoni hapo kwa ajili ya uhakiki.

Sauti ya kamanda wa polisi mkoa wa Mara

Wakati huo huo, baadhi ya wakazi wa eneo la Manyamanyama wamesema jengo hilo limekuwa limetelekezwa kwa miaka kadhaa na hutumiwa kama maficho ya watu mbalimbali. Wamezitaka mamlaka kulifanyia hatua stahiki ili kuondoa hatari zinazoweza kujitokeza.

Sauti za Baadhi ya wananchi