Mazingira FM
Mazingira FM
27 July 2026, 4:29 pm

Msaada huo umetolewa kufuatia ombi lililowasilishwa na uongozi wa kanisa hilo.
Na Adelinus Banenwa
Katibu wa Mbunge wa Jimbo la Bunda Mjini, Mariam Amosi, kwa niaba ya Mhe Mbunge Esther Bulaya, leo Julai 27, 2026, amekabidhi mabati bando mbili zenye thamani ya shilingi 700,000 kwa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Mugaja Manyamanyama.
Msaada huo umetolewa kufuatia ombi lililowasilishwa na uongozi wa kanisa hilo, uliolenga kuomba mchango wa kusaidia ujenzi wa nyumba ya ibada.
Akizungumza baada ya kupokea msaada huo, mzee wa Kanisa la KKKT Mugaja, Tito Mashini, alimshukuru Mbunge Esther Bulaya kwa moyo wa kujitolea kusaidia maendeleo ya kanisa. Alieleza kuwa mabati hayo yatasaidia hatua ya sasa ya ujenzi, ambayo ni kupaua jengo la kanisa, ili waumini waweze kupata sehemu bora na salama ya kuabudia.
Kwa niaba ya waumini wa kanisa hilo, Tito Mashini aliahidi kuyaelekeza mabati hayo katika matumizi yaliyokusudiwa na kuendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kukamilisha ujenzi wa kanisa.