

14 June 2025, 4:29 pm
Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Evans Alfred Mtambi na Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Bunda Charles Manumbu,Piacha na Thomas Masalu
Ameitaka Halmashauri hiyo kuongeza vyanzo vya ndani vya mapato na kufanya upembuzi yakinifu katika shughuli za uchimbaji madini na uwekezaji uliofanyika katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti
Na Thomas Masalu
Mkuu wa Mkoa wa Mara Mhe. Evans Alfred Mtambi ameagiza Halmashauri ya Wilaya ya Bunda iwasilishe mkakati wa kukusanya shilingi milioni 700 za mapato ya ndani kufikia Juni 30, 2025.
Mhe. Mtambi ametoa agizo hilo katika kikao maalum cha Baraza la Madiwani kwa ajili ya kujadili hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) 13 juni, 2025 baada ya Halmashauri hiyo kukusanya shilingi bilioni 1.8 ya mapato ya ndani hadi tarehe 31 Mei, 2025 ambayo ni sawa na asilimia 75 ya lengo la kukusanya shilingi bilioni 2.5 katika mwaka wa fedha 2024/2025.
Mhe. Mtambi ameitaka Halmashauri hiyo kuongeza vyanzo vya ndani vya mapato na kufanya upembuzi yakinifu katika shughuli za uchimbaji madini na uwekezaji uliofanyika katika Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ili kuifanya halmashauri hiyo kuwa na nguvu ya kiuchumi yitakayowahakikishia ustawi wa wananchi wa Halmashauri hiyo.
Katika hatua nyingine, Mhe. Mtambi amewaonya viongozi wa kata na vijiji wanaojihusisha na uvuvi haramu kuchukuliwa hatua za kisheria na kuongeza kuwa nafasi zao sio kichaka cha kuficha uovu huo na Serikali itawachukulia hatua za kisheria.