Mazingira FM

Anayetuhumiwa kubaka, kulawiti mwanafunzi apandishwa kizimbani Bunda

21 March 2024, 7:20 pm

Picha na Adelinus Banenwa

Bunda: Mwalimu aliyetuhumiwa kubaka, kulawiti mwanafunzi apandishwa kizimbani akana mashtaka arudishwa rumande

Na Adelinus Banenwa

Leo tarehe 21/03/2024 katika mahakama  ya Wilaya Bunda amepandishwa kizimbani Vicent Joseph Nkunguu umri miaka  36 mwalimu mkuu shule ya msingi Masahunga kwa tuhuma za  kujaribu kuua, kulawiti na ubakaji.

Kesi ya kwanza inayomkabili ni kesi namba 7623/2024 ambayo ni kujaribu kuua  kinyume na kifungu cha 211 (a) cha kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2022.

Kesi ya pili yenye makosa mawili ambayo ni kubaka kinyume na kifungu cha 130 (1), (2) (e) na kifungu cha 130 (1) cha kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2022  na kulawiti kinyume na kifungu cha 154 (1) cha kanuni ya adhabu sura ya 16 marejeo ya mwaka 2022.

Awali akisoma  mashtaka yanayomkabili mtuhumiwa huyo  mbele ya Hakimu Mkazi mwandamizi wa mahakama  Betron Sokanya , mwendesha mashtaka wa polisi Athuman Salimu alieleza mahakama kuwa mshtakiwa alitenda kosa hilo tarehe 09/03/2024  majira ya usiku kwa kumbaka, kumlawiti na kujaribu kumuua kwa lengo la kupoteza  ushahidi  mwanafunzi wa darasa la sita shule ya msingi Masahunga (16) jina limehifadhiwa.

Katika kesi ya kwanza mshitakiwa hakutakiwa kujibu lolote kwani mahakama haikuwa na mamlaka ya kusikiliza shauri hilo.

Na katika kesi ya  pili mshtakiwa alikana makosa yote mawili ambapo hakimu aliamuru mtuhumiwa kurudishwa  rumande hadi tarehe 03/04/2024 kesi  hiyo itakapotajwa tena kwa kuwa mshtakiwa hakukidhi masharti ya dhamana.