Mazingira FM
Mazingira FM
15 July 2026, 5:56 pm

Kaminyoge amesisitiza kuwa vyandarua hivyo ni salama kwa matumizi ya binadamu na kuwataka wananchi kupuuza taarifa za upotoshaji kuhusu matumizi yake, ikiwemo madai kuwa vinaweza kusababisha kupungua kwa nguvu za kiume.
Na Mariam Mramba
Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Enock Kaminyoge, amewaagiza Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri zote ndani ya wilaya hiyo kusimamia kwa uadilifu, uwazi na uaminifu zoezi la kitaifa la ugawaji wa vyandarua vyenye dawa ya muda mrefu ili kuhakikisha vinawafikia wananchi wote.
Kaminyoge ametoa agizo hilo leo, Julai 15, 2026, wakati wa uzinduzi wa zoezi hilo uliofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.

Amesema tofauti na kampeni zilizopita, safari hii vyandarua vitagawiwa kwa wananchi wote watakaojiandikisha kwenye daftari la kaya, huku akiwahimiza wananchi kujitokeza kwa wingi ili waweze kunufaika na mpango huo wa Serikali wa kudhibiti ugonjwa wa malaria.
Kaminyoge amesisitiza kuwa vyandarua hivyo ni salama kwa matumizi ya binadamu na kuwataka wananchi kupuuza taarifa za upotoshaji kuhusu matumizi yake, ikiwemo madai kuwa vinaweza kusababisha kupungua kwa nguvu za kiume.

Aidha, amewatahadharisha wananchi kuacha kutumia vyandarua hivyo kwa shughuli nyingine kama kuvulia dagaa na samaki wadogo, kuweka uzio wa bustani au kufugia vifaranga, akisema matumizi hayo yanakwamisha juhudi za Serikali za kupambana na malaria.
Katika hatua nyingine, Mkuu huyo wa Wilaya amewataka viongozi wa ngazi zote kushirikiana na watendaji wa vijiji, mitaa na kata kuimarisha usafi wa mazingira ili kupunguza mazalia ya mbu, akibainisha kuwa taka za plastiki na karatasi zinazotupwa ovyo ni miongoni mwa chanzo cha uchafuzi wa mazingira.