Mazingira FM
Mazingira FM
15 July 2026, 5:29 pm

Akemea tabia ya baadhi ya wanachama wa vikundi kwenda benki kuchukua mikopo bila kuwashirikisha wenzao, akisema mwenendo huo husababisha migogoro ndani ya vikundi.
Na Mariam Mramba
Mbunge wa Jimbo la Bunda, Boniphace Getere, amesema atashirikiana kwa karibu na Benki ya NMB pamoja na Benki ya Azania ili kuhakikisha wananchi wa jimbo lake, hususan wajasiriamali, wanapata mikopo yenye riba nafuu na masharti rafiki yatakayowasaidia kukuza shughuli zao za kiuchumi.
Getere ametoa kauli hiyo leo, Julai 14, 2026, alipokuwa akizungumza katika kikao maalum cha utoaji elimu kwa wajasiriamali wadogo kilichowakutanisha wadau mbalimbali, wakiwemo wenyeviti wa vijiji, watendaji wa vijiji, viongozi wa kata, wataalamu kutoka Halmashauri ya Wilaya ya Bunda pamoja na wadau wa maendeleo kutoka Benki ya NMB na Benki ya Azania.
Mbunge huyo ameziomba benki hizo kuhakikisha haziwacheleweshi wajasiriamali waliokamilisha taratibu zote za kupata mikopo. Amesema si sahihi vikundi vinavyotekeleza wajibu wao kuathiriwa na vikundi vya maeneo mengine vinavyoshindwa kurejesha mikopo kwa wakati, kwani hali hiyo inawanyima fursa ya kuongeza uzalishaji na kukuza biashara zao.
Aidha, Getere amekemea tabia ya baadhi ya wanachama wa vikundi kwenda benki kuchukua mikopo bila kuwashirikisha wenzao, akisema mwenendo huo husababisha migogoro ndani ya vikundi na kuwanyima wanachama wengine haki ya kunufaika na mikopo hiyo.
Baadhi ya wajasiriamali waliohudhuria mafunzo hayo wamemuomba Mbunge huyo kuwasaidia kuharakisha upatikanaji wa mikopo kwa wale ambao tayari wamekamilisha taratibu zote za maombi katika benki husika.
Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ameeleza kuwa ili mwananchi aweze kupata mkopo ni lazima awe na shughuli halali ya kiuchumi inayomwingizia kipato, ameongeza kuwa mikopo hiyo ina riba nafuu, lakini haitawahusu viongozi walioko madarakani, watumishi wa serikali pamoja na wastaafu wanaopokea pensheni.
Naye Afisa Mahusiano wa Benki ya Azania, David Maliba, alisema ucheleweshaji wa utoaji wa mikopo kwa baadhi ya vikundi unatokana na vikundi vingine kushindwa kumaliza madeni yao kwa wakati, hali ambayo huathiri mzunguko wa utoaji wa mikopo kwa waombaji wengine.