Mazingira FM

Wazazi, walezi Bunda waitikia chanjo saratani mlango wa kizazi

23 April 2024, 11:05 am

Wahudumu wa afya Bunda wakiendelea na zoezi la uchanjaji, Picha na Riwina Mnamba

Watoto wa kike miaka 9 – 14 wapatao 11,650 wilayani Bunda wapata chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi (HPV) siku ya uzinduzi April 22, 2024

Na Adelinus Banenwa

Zaidi ya watoto wa kike miaka 9 hadi 14 wapatao 41370 wilayani Bunda wanatarajiwa kupata chanjo ya saratani ya mlango wa kizazi katika kampeini maalumu ya serikali iliyoanza April 22 hadi april 26, 2024 .

Baadhi ya watoto shule ya msingi Miembeni wakifuatilia maelekezo kutoka kwa wataalamu wa afya kabla zoezi la chanjo kuanza, Picha na Riwina Mnamba

Dr Hamidu Adinani mganga mkuu wa halmashauri ya wilaya ya Bunda akizungumza na Mazingira Fm amesema kwa halmashari yake wanatarajia kuwachanja watoto wapatao 23,994 kupitia kampeini hiyo ya serikali huku kwa siku ya kwanza ya uzinduzi wamefanikiwa kuwachanja watoto elfu sita (6000) .

Dr Hamidu amesema chanjo hiyo inatolewa kwa watoto wenye umri huo kutokana na kwamba utafiti wa serikali umebaini kuwa katika umri wao wanakuwa bado hawajaanza masuala ya kujamiiana hivyo inawafanya kuwa walengwa wa hiyo chanjo, Pia amebainisha kuwa madhara ya saratani ya mlango wa kizazi hujitokeza kwa mwanamke anapofikisha miaka 30 na kuendelea na hiyo chanjo inawafanya wasipate maambukizi ambayo hupatikana kwa njia ya kujamiiana.

Naye Dr Yusuph Steven Wambura kaimu mganga mkuu halmashauri ya mji wa Bunda amesema kwa halmashauri ya mji wa Bunda wao wanalengo la kuwachanja wasichana lengwa wapatao 17376 huku siku ya uzinduzi wamechanja watoto 5650 wakati malengo yao yakiwa ni 3475 hivyo kuwa juu ya malengo tarajiwa.

Dr Yusuph Steven Wambura kaimu mganga mkuu halmashauri ya mji wa Bunda, Picha na Riwina Mnamba

Dr Yusuph ameongeza kuwa wazazi na walezi hawatakiwi kuwa na hofu na chanjo hiyo kwa kuwa ni salama na imethibitishwa na wizara ya afya kwa matumizi,  na lengo lake ni kumkinga mtoto wa kike dhidi ya ugonjwa huo wa saratani ya mlango wa kizazi ambao hauna tiba.