Mazingira FM

Serengeti yaendelea kung’ara hifadhi bora barani Afrika

1 January 2024, 9:10 pm

Hifadhi ya Taifa ya Serengeti imejipanga kuendelea kuboresha huduma mbalimbali ili kuwavutia watalii na kuifanya kuendelea kuwa hifadhi bora ya kwanza barani Afrika.

Hayo yamesemwa na Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, Kamishna Msaidizi wa Hifadhi Moronda B. Moronda wakati wa hafla ya kupokea Tuzo ya tano mfululizo ya Hifadhi Bora Barani Afrika ‘African Leading National Park 2023’ iliyofanyika leo katika eneo la Seronera Mbugani Serengeti.

Moronda amesema kwasasa wanaendelea kuboresha sehemu za malazi, miundombinu ya barabara, viwanja vya ndege pamoja na ulinzi mkubwa wa maliasili ili kuifanya hifadhi hiyo kuwa bora wakati wote.

Kamishina Msaidizi wa Hifadhi ya Taifa Serengeti, Moronda B. Moronda (wakwanza kushoto mwenye kofia na t-shirt nyeupe) akionesha tuzo kwa watalii katika eneo la Seronera-Serengeti
Moronda B. Moronda

Awali akikabidhi tuzo hiyo iliyotolewa kampuni ya Tripadvisor inayoshushughulika na kutoa mrejesho wa mahoteli na vivutio mbalimbali duniani, Afisa Uhifadhi Mkuu Kitengo cha Maendeleo ya Biashara TANAPA, Augustine Massesa amesema ushindi huo ni ishara ya ushirikiano mzuri kati ya wadau wote wa sekta ya utalii na juhudi za Rais wa Tanzania, Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassani

Afisa Uhifadhi Mkuu kitengo cha Maendeleo ya Biashara TANAPA, Augustine Massesa akiwasili uwanja wa ndege Seronera mbugani Serengeti kukabidhi Tuzo kwa SENAPA
Augustine Massesa

Naye Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Dr Vicent Mashinji amesema kwa upande wao wataendelea kuimarisha hali ya ulinzi na usalama ili kuhakikisha shughuli zote za utalii zinaendelea vizuri katika Hifadhi ya Serengeti.

Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Dr. Vicent Mashinji
Dr. Vicent Mashinji