Mazingira FM

Manusura ajali ya mitumbwi Bunda wasimulia hali ilivyokuwa

31 July 2023, 8:52 pm

Pichani ni Baraka Jumbula wa kwanza kushoto na Joseph Kundi wa pili kulia ambao ni manusura wa ajali ya mitumbwi. Picha na Adelinus Banenwa

Vijana walionusurika kwenye ajali ya mitumbwi eneo la Mchigondo Bunda wasimulia hali ilivyokuwa baada ya mitumbwi kuzama na wao walivyonusurika huku wakiokoa watoto watatu.

Na Adelinus Banenwa na Edward Lucas

Joseph Kundi mkazi wa Bulomba alikuwa ni miongoni mwa wasafiri katika mitumbwi iliyozama ziwa Victoria eneo la Mchigondo Bunda ambaye katika tukio la kuzama anasimulia juhudi alizozifanya za kuogelea na kujaribu kuwaokoa watu waliokuwa wamezama katika mtumbwi wa kwanza kabla ya dakika chache mtumbwi wao pia kuzama.

Anasema wakiwa nyuma waliona mtumbwi wa mbele unazama na watu waliokuwa ndani yake walianza kupiga kelele kuomba msaada ambapo walifanya jitihadi za kuwahi ili kuokoa na waliposogea karibu alijitosa ndani ya maji ili kusaidia hasa watoto waliokuwa wakielea ndani ya maji.

Akiwa katika jitihada hizo kwa kushirikiana na mmoja kati ya vijana waliokuwa wamezama katika mtumbwi huo alifanikiwa kuwaokoa baadhi ya watu na kuwahamishia katika mtumbwi wao lakini dakika chache baadaye mtumbwi wa pili pia ulizidiwa na idadi ya watu na purukushani za watu wengine kujiokoa jambo lililopelekea mtumbwi huo kuzama.

Baada ya mitumbwi yote miwili kuzama Joseph anasimulia zaidi nini kilifanyika ili kujiokoa na kubahatika kuwaokoa watoto wengine watatu kwa kushirikiana na Baraka Jumbula aliyekuwa katika mtumbwi wa kwanza.

Sauti ya Joseph Kundi na Barka Jumbula manusura ajali ya mitumbwi kuzama wakisimulia tukio