Mazingira FM

RC Mara, awatimua makatibu wa wabunge kwenye kikao akisema kisheria siyo wajumbe.

30 November 2022, 7:29 am

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Meja Jenerali Suleiman Mzee amewaondoka kwenye kikao cha Bodi ya Barabara ya Mkoa huo makatibu wa wabunge ambao waliwawakilisha wabunge kwa maelezo kuwa makatibu hao siyo wajumbe halali wa kikao hicho huku akidai wabunge wengi wa mkoa huo wamekuwa na dharau na hawahudhurii vikao vya kisheria.

Mkuu huyo wa mkoa amefanya maamuzi hayo leo Jumanne Novemba 29, 2022 muda mfupi kabla ya kuanza kwa kikao hicho ambacho kimefanyika ukumbi wa uwekezaji mjini Musoma na kusema makatibu wa wabunge sio wajumbe halali wa kikao hicho.

Amesema kwa muda mrefu wabunge wa Mkoa wa Mara wamekuwa na tabia ya kutokuhudhuria vikao ambavyo vipo kisheria jambo ambalo amedai ni dharau na kwamba halikubaliki.

“Haya ni mazoea mkoa huu una wabunge 10 wa majimbo pamoja na wale wa viti maalum, lakini wabunge mara zote hawahudhurii vikao hivi kwa hali hii hatuwezi kufika wanashindwa kuhudhuria vikao kwaajili ya maendeleo ya mkoa hii haikubaliki” amesema na kuongeza

“Mimi siwezi kumleta katibu wangu hapa aendeshe hiki kikao maana kama ni katibu hata mimi pia ninaye. Hakuna kitu kama hicho kila mtu kwa nafasi yake atimize wajibu wake na kwa yule mwenye udhuru atoe taarifa. Niwaombe wabunge waheshimu vikao hivi ambavyo vipo kisheria, kwanza vinawasaidia hata wao,” amesema.

Akichangia kuhusu uamuzi huo, katibu wa CCM Mkoa wa Mara, Lengael Akyoo amesema anaunga mkono uamuzi huo kwani wabunge wa mkoa huo ambao wengi wao wanatokana na chama hicho, wamekuwa na tabia ya kutokuhudhiria vikao vinavyofanyika mkoani humo.

“Sijawahi kusikia katibu wa mbunge amemuwakilisha mbunge bungeni lakini inapofika kwenye vikao tena vya kisheria, wakati wote wanawatuma makatibu wao hivi katibu anaweza kuwasilisha hoja za mbunge wake? Hii haikubaliki?” amesema.
Amesema umefika muda wabunge hao wanatakiwa kuheshimu sheria na kuhudhuria vikao ambavyo vinafanyika ndani ya mkoa huo kwa lengo la kujadili na kuweka mikakati ya pamoja kwa ajili ya maendeleo ya mkoa wa Mara.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Dkt Vincent Mashinji amesema kitendo cha wabunge kutohudhuria kikao hicho ni cha makusudi kwani wengi wao wapo majimboni wanaendelea na mambo yao. “Wengine wako mitaani, wengine tumepishna nao,” amesema.

 

Wabunge ambao hawakuonekana kikaoni hadi wakati Mkuu wa Mkoa anachukua hatua hiyo ni Vedastus Mthayo wa Musoma Mjini, Profesa Sospeter Muhongo (Musoma Vijijini), Jumanne Sagini (Butiama), Robert Maboto (Bunda Mjini), Charles Kajege (Mwibara), Amsabi Mrimi (Serengeti), Mwita Waitara (Tarime Vijijini), Michael Kembaki (Tarime Mjini), Jafari Chege (Rorya), Ghati Chomete (Viti Maalum) na Agnes Marwa (Viti Maalum).

 

Mwenyekiti mpya wa CCM Mkoa wa Mara, Patrick Chandi Marwa amehudhuria kwa mara ya kwanza kikao hicho.