Mazingira FM

Bunda: Aliyezikwa aonekana tena, ndugu wapigwa na butwaa

17 February 2024, 8:35 pm

Maajabu aliyezikwa baada ya ndugu kupata taarifa za kifo chake aonekana tena, wakazi wa eneo hilo wapigwa na butwaa wakidhani ni mzimu.

Na Adelinus Banenwa

Maajabu aliyezikwa baada ya ndugu kupata taarifa za kifo chake aonekana tena wakazi wa eneo hilo wapigwa na butwaa wakidhani ni mzimu.

Ni tukio lililoacha wakazi wa Mcharo wilayani Bunda midomo wazi baada ya kumaliza matanga ya aliyedaiwa ni ndugu yao kuonekana tena akiwa mzima.

Ratifa Msafiri Mangu 28 mkazi wa mtaa Mcharo kata ya Mcharo Halmashauri ya mji wa Bunda mkoani Mara ambaye amekuwa habari kubwa kwa wakazi wa maeneo hayo ya Mcharo alipofika nyumbani kwa kutoka kwenye harakati za utafutaji wa maisha na kukuta historia nyingine nyumbani kwao kuwa tayari amezikwa wiki moja imepita.

Tukio hilo la kushangaza limetokea tarehe 10 Feb 2024 ambapo inaelezwa kuwa Ndugu wa Ratifa baada ya kumaliza matanga wakiwa wamekaa nje ya nyumba yao majira ya saa 10 za jioni walimuona Ratifa anakuja gafla wakashtuka na kutaka kukimbia wakidhani ni mzimu lakini baadae alisimama kwa mshangao huku wakitahadharishana kutomgusa.

Rose Muhoja mama mkubwa wa Ratifa amesema hatua ya kwanza walimpigia mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa Mcharo ambaye alionekana kushtushwa na taarifa hizo na alipofika kwa kushirkiana na familia walikubaliana Ratifa asiguswe na wanafamilia wala asiingie kwao hadi afanyiwe mila na matambiko ndipo aruhusiwe.

Kwa upande wake Ratifa Msafiri ameiambia Mazingira Fm kuwa yeye tangu alipoondoka kwao mnamo 26 Dec 2023 hakujua nini kinaendelea kwa kuwa akiwa mjini Bunda aliibiwa simu na begi lake la nguo hali iliyopelekea kukosa mawasiliano na familia na kwa muda huo hakuwa na namba ya mtu yeyote kutoka kwao.

” Sikuwa na mawasiliano na mtu kutoka nyumbani maana simu yangu ambayo ilikuwa na line ya mama na begi la nguo viliibiwa nikiwa Bunda mjini hivyo nilielekea visiwani kwenye kisiwa kimoja kiko mpakani mwa Tanzania na Uganda”.

Ratifa ameendelea kuelezea kuwa ” nilishangaa siku ya Jmosi tarehe 10 Feb wakati nakaribia nyumbani vijana wawili wa bodaboda aliponiona nakuja nikiwa nimebebwa kwenye pikipiki walishangaa wakaja wamenifuata kwa nyuma wakiniambia wewe kumeshakuzika umerudije au ni mzimu? nilibaki na mshangao!!! Nimekufa!? Nimezikwa!?

“Nilipofika nyumbani nikaona kila mmoja ananikimbia hata mwanangu wakamkataza asinishike watu wengi wakaja kuniona wengi wao wakisema ni mzimu kwani anaongea uwenda ni bubu tayari kwa kweli kila mmoja alikuwa anazungumza la kwake.”

Ratifa amesema jambo hili limemuathiri pakubwa hasa kisaikolojia maana hadi sasa kuna watu hawaamini kama kweli ni yeye licha ya kuwaambia kwamba hajafa Kila siku watu wanakuja kuona kama kweli yupo ama uwenda akatoweka kimiujiza.

Tukio la mazishi ya mtu aliyesadikiwa kuwa ni Ratifa

Awali tarehe 9 Jan 2024 lilipotiwa tukio la mwili wa mwanamke kuonekana kandokando ya ziwa Victoria eneo la mtaa wa Tamau kata ya Nyatwali wilayani Bunda ambapo baada ya jeshi la polisi kufanya taratibu zake waliwaruhusu wakazi wa Tamau kuzika mwili huo baada ya kukosa ndugu.

Mnamo Jan 27 familia ya Ratifa kwa kibali Cha serikali ilifika Tamau ili kufukua na kubeba mwili wa mtu huyo wakidai ni Ndugu yao (yaani Ratifa) baada y maelekezo ya mashuhuda waliohusika na mazishi pale Tamau.

Ndugu hao walidai binti yao (Ratifa) tangu alipoondoka nyumbani kwao tarehe 26 Dec hakuwahi kupatikana tena na aliondoka akidai anaelekea Nyatwali na Kwa namna mashuhuda walivyoelezea nguo na namna alivyokuwa amevaa imetosha kuamini kwamba ni kweli alizikwa mahali pale ni ndugu yao hayo yalikuwa maneno ya Rose Muhoja mama mkubwa wa Ratifa.

Ufukuaji wa kabuli na uhamishaji wa mwili huo ulisimamiwa na viongozi wa kata akiwepo mtendaji wa kata ya Nyatwali, mwenyekiti wa mtaa wa Tamau, mwenyekiti wa mtaa wa Mcharo pia mwakilishi kutoka ofisi ya Afisa afya Halmashauri ya Mji wa Bunda.

Maamuzi ya Serikali baada ya Ratifa kuonekana

Ofisi ya mkuu wa wilaya ya Bunda kupitia kwa katibu tawala wilaya Salumu Mtelela ameitaka familia ya Ratifa kuhamishia mwili waliouzika kwenye makabuli ya umma kwa gharama zao ambopo kimsingi hawezi kwao kwa kuwa hakuwa ndugu yao inaweza kuendelea kuleta taharuki kwa watu endapo kabuli hilo vitaendelea kubaki kwenye familia hiyo.