Mazingira FM

Mzee wa miaka (62) ahukumiwa miaka 30 jela kwa kosa la ubakaji

12 November 2023, 11:00 am

Mahakama ya wilaya ya Bunda imemuhukumu Nyakurunduma Matutu kuboja (62) mkazi Kiroreli kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka kumi.

Na Adelinus Banenwa

Mahakama ya wilaya ya Bunda imemuhukumu Nyakurunduma Matutu kuboja (62) mkulima na mkazi wa kijiji cha Kiroreli mtaa wa kambubu miaka 30 jela kwa kosa la kumbaka mtoto mwenye umri wa miaka kumi mwanafunzi wa darasa la nne.

Akisoma hukumu hiyo Hakimu mkazi mwandamizi Mheshimiwa Betron Sokanya alieleza kuwa upande wa mashtaka umethibitisha kosa hilo bila kuacha shaka yo yote baada kuita mashahidi wanne akiwemo Daktari aliyethibisha kubakwa kwa mtoto huyo.

Awali ilielezwa na mwendesha Mashtaka wa serikali Athuman Salimu  kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa hilo 21/04/2023 majira ya mchana nyumbani  kwa mshtakiwa wakati mtoto huyo anatoka shule,ambapo mshtakiwa alimuita na kumuingiza ndani kwake kisha kumfanyia unyama huo mtoto huyo kinyume na kifungu cha 130 (1)(2) (e) na kifungu cha 131(1) cha kanuni ya adhabu sura 16 marejeo ya sheria ya mwaka 2022.

Mwendesha mashtaka Athumani aliiomba mahakama itoe adhabu kali kwa mshtakiwa bila huruma kwani vitendo vya ubakaji vimekithiri katika jamii ili iwe fundisho.

Katika utetezi wake mshtakiwa aliamua kunyamaza kimya

Ndipo Hakimu Sokanya alipotamka kuwa mshtakiwa atatumikia kifungo jela miaka thelathini na baada ya kifungo hicho amlipe fidia muhanga kiasi cha shilongi milioni moja na laki tano.