Mazingira FM

Miezi 3 tangu zahanati izinduliwe haijaanza kazi, wananchi wapaza sauti

12 October 2023, 5:14 pm

Jengo la Zahanati mtaa wa Kung’ombe ambalo lilizinduliwa mwezi July 2023. Picha na Edward Lucas

Zahanati ilizinduliwa na mbio za Mwenge wa Uhuru Julai 11 2023 lakini hadi sasa Oktoba 2023 bado haijaanza kazi, wananchi wapaza sauti kwa serikali.

Na Edward Lucas

Wakazi wa mtaa wa Kung’ombe Halmashauri ya Mji wa Bunda mkoani Mara wameiomba serikali iharakishe kuanza utoaji wa huduma ya afya katika zahanati ambayo ilizinduliwa na mbio za Mwenge miezi mitatu iliyopota.

Wakizungumza na Radio Mazingira Fm kwa nyakati tofauti wakazi hao wamesema tangu ulipoanza mpango wa ujenzi wa zahanati hiyo walijitoa kwa hali na mali ili kuepuka adha ya adha ya upatikanaji wa huduma za afya katika mtaa huo na maeneo jirani lakini matumaini hayo yanazidi kufifia baada ya kuona siku zinaenda na hakuna huduma zinazotolewa hadi sasa.

Zahanati ya Kung’ombe iliyojengwa kwa ushirikiano wa wananchi na serikali. Picha na Edward Lucas

Wamesema kutokana na kukosekana huduma wamekuwa wakipitia changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na kutembea mwendo mrefu ili kupata huduma za afya na hivyo wameiomba serikali iharakishe mchakato wa kuanza kutoa huduma ili iwapunguzie adha hiyo.

Sauti ya wakazi wa mtaa wa Kung’ombe

Mary Reuben Magese na Yakobo Zabron Ndoroba ambao ni wajumbe wa serikali ya mtaa wa Kung’ombe wamekiri kupokea malalamiko ya wananchi wakihoji kuhusu kuanza huduma kama ilivyoahidiwa wakati wa uzinduzi wa zahanati kupitia mbio za Mwenge wa Uhuru July 11, 2023 na kubainisha juhudi zilizofanyika katika kufanikisha ujenzi huo.

Yakobo Zabron, mjumbe serikali ya mtaa wa Kung’ombe. Picha na Edward Lucas
Sauti ya Wajumbe wa serikali ya mtaa

Kufuatia hatua hii, Mazingira Fm amemtafuta Mwenyekiti wa mtaa wa Kung’ombe, Khamis Malunde ili kujua ni kwa namna gani wanashughulia kilio cha wananchi ambapo amekiri kuwepo malalamiko hayo na kueleza kuwa amewahi kuyafikisha ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri na kuahidiwa kushughulikiwa lakini hadi sasa haoni utekelezaji.

Khamis Malunde, mwenyekiti mtaa wa Kung’ombe. Picha na Edward Lucas
Sauti ya Khamis Malunde

Kwa mujibu wa taarifa ya ujenzi wa zahanati iliyosomwa mbele ya kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru mnamo tarehe 11 July 2023, Abdalla Shaib Kaim ilisema mradi uligharimu jumla ya shilingi Mil 69.679 ambapo kati ya fedha hizo Mil 50 ilitokana na mapato ya ndani ya Halmashauri na michango ya wananchi ni shilingi Mil 19.676

Ambapo taarifa hiyo ilisema lengo la mradi ni kuwasaidia wananchi mitaa yote iliyojirani na mtaa wa Kung’ombe kupunguza vifo vya watoto na akina mama wakati wa kujifungua kwa kukosa huduma za afya jirani.

Naye Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru, Abdalla Shaib Kaim katika hotuba yake iliyoitoa katika viwanja vya zahanati hiyo mnamo tarehe 11 July 2023 sambamba na kupongeza juhudi za Ujenzi wa zahanati ilitoa siku 7 kufanyiwa marekebisho baadhi ya dosari na kueleza kuwa itapendeza kuanzia mwezi Agosti 2023 mapema mradi uanze kazi ili wananchi wapate huduma.