Mazingira FM

Bulaya awashika mkono kituo cha kulea watoto yatima Bunda

18 July 2023, 9:42 pm

Mbunge Viti Maalumu Mh. Ester Bulaya akisalimiana na watoto kituo St. Francis kilichopo Balili-Bunda. Picha na. Edward Lucas

Bulaya atembelea kituo cha watoto yatima na mazingira magumu St. Francis na kusaidia mahitaji mbalimbali kama sukari, mchele, unga na mafuta

Na Edward Lucas

Mbunge wa Viti Maalumu na ambaye pia amewahi kuwa Mbunge wa Bunda Mjini, Mh Ester Amos Bulaya leo ametembelea kituo cha kulelea watoto yatima St. Francis kilichopo mtaa wa Rubana kata ya Balili wilaya ya Bunda Mkoani Mara na kutoa mahitaji mbalimbali kwa ajili ya watoto.

Akizungumza baada ya zoezi hilo la kukabidhi Mchele, Unga, Sukari, Mafuta na mahitaji mengine Mh Ester amesema watoto hao wanahitaji upendo, ushirikiano na kutembelewa ili wapate moyo wa kuona kupoteza wazazi na kuwa katika changamoto ya mazingira magumu sio sababu ya kutotimiza ndoto zao.

Sauti ya Mbunge Ester Bulaya baada ya kukabidhi mahitaji kituo cha St. Francis

Katika ziara hiyo ambayo ilitoa nafasi ya watoto kuimba na kuuliza maswali mbalimbali kwa lengo la kupata motisha katika makuzi yao iliwapa nafasi pia watoto kutaka kujua kazi za mbunge na vipaumbele vyake katika kusimamia shughuli za maendeleo.

Sauti ya Ester Bulaya kuhusu maswali aliyokutana nayo kwa watoto

Kwa upande wake Kiongozi wa Kituo hicho, Sr Arta Lleshaj ameshukuru kwa kupokea mahitaji hayo na kuiomba jamii kuendelea kuwa karibu na watoto hao kwani bado wanamahitaji mengi.

Watoto wa kituo cha St. Francis wakiwa na Sr. Arta wakimsikiliza mgeni wao Mh Ester bulaya
Sauti ya Sr Arta akitoa neno la shukurani na kubainisha watoto wanaolelewa katika kituo hicho