Mazingira FM

Matumizi ya pombe miongoni chanzo cha ukatili

12 July 2026, 1:28 pm

Msimamizi wa Miradi wa ICCAO, Maria Mrindoko

Utafiti uliofanyika Januari mwaka huu umeonyesha kuwa asilimia 34.7 ya washiriki waliripoti kufanyiwa ukatili na mtu aliyekuwa chini ya ushawishi wa pombe.

Na Edward Lucas

Matumizi yaliyokithiri ya pombe yameendelea kutajwa kuwa miongoni mwa vihatarishi vinavyoongeza matukio ya ukatili wa kijinsia, huku yakisababisha pia watoto kukosa mahitaji muhimu na kudhoofisha ustawi wa familia.

Shirika la ICCAO linalotekeleza mradi wa miaka mitatu wa “Ulevi Sio Dili” mkoani Mara kuanzia mwaka 2026 hadi 2028 limesema utafiti wake wa awali umebaini kuwa pamoja na athari za kiafya na kiuchumi, matumizi yaliyokithiri ya pombe yanahusishwa na ongezeko la vitendo vya ukatili wa kijinsia, uhalifu na changamoto za malezi.

Sauti ya Msimamizi wa Miradi wa ICCAO, Maria Mrindoko

Msimamizi wa Miradi wa ICCAO, Maria Mrindoko, akizungumza na Radio Mazingira Fm amesema utafiti uliofanyika Januari mwaka huu umeonyesha kuwa asilimia 34.7 ya washiriki waliripoti kufanyiwa ukatili na mtu aliyekuwa chini ya ushawishi wa pombe, huku vipigo na mashambulio vikiongoza.

Aidha, amesema matumizi yaliyokithiri ya pombe yamekuwa yakichangia pia matukio mengine kama ubakaji, wizi na migogoro ya kifamilia.

Kwa mujibu wa ICCAO, athari hizo haziishii kwa wahanga wa ukatili pekee, bali huwafikia pia watoto, ambapo baadhi hukosa mahitaji muhimu ya elimu na malezi kutokana na wazazi au walezi kutumia muda na rasilimali nyingi katika matumizi ya pombe.

Sauti ya Msimamizi wa Miradi wa ICCAO, Maria Mrindoko

Hata hivyo, ICCAO imesisitiza kuwa suluhisho linahitaji ushiriki wa jamii kwa kuimarisha malezi, kuwasaidia vijana kujishughulisha na shughuli za kiuchumi, kusimamia sheria za matumizi ya pombe na kutoa elimu kwa wauzaji pamoja na watumiaji ili kupunguza athari zinazotokana na matumizi yaliyokithiri ya pombe.

Shirika hilo pia limeeleza kuwa kampeni ya “Ulevi Sio Dili” hailengi kuzuia watu kunywa pombe, bali kuhamasisha matumizi yenye uwajibikaji na kupunguza madhara yanayoweza kuhatarisha afya, familia na usalama wa jamii.

Sauti ya Msimamizi wa Miradi wa ICCAO, Maria Mrindoko

Vilevile limewataka watu wenye changamoto ya uraibu kutafuta msaada mapema, likieleza kuwa mabadiliko yanawezekana kwa kujitambua, kujiepusha na mazingira yanayochochea matumizi mabaya ya pombe na kupata huduma stahiki.