

16 May 2025, 2:16 pm
Ni wajibu wa baraza la madiwani kujua miradi inayotekelezwa katika maeneo yao na kuisimamia ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika.
Na Adelinus Banenwa
Katibu tawala wilaya ya Bunda Ndugu Salumu Mtelela ameitka halmashauri ya wilaya ya Bunda kukamilisha miradi inayoendelea kutekelezwa katika halmashauri hiyo kwa fedha za serikali kuu au za mapato ya ndani.
Mtelela amesema hayo kwenye kikao cha baraza la madiwani halmashauri ya wilaya ya Bunda cha robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2024 na 2025 kilichofanyika tarehe 16 May 2025.
Mtelela amesema ni wajibu wa baraza la madiwani kujua miradi inayotekelezwa katika maeneo yao na kuisimamia ili kuhakikisha miradi hiyo inakamilika
Mbali na hilo pia Mtelela amehimiza baraza hilo kuongeza vyanzo vya mapato ya halmashauri ili kuwezesha miradi inayotekelezwa kwa mapato ya ndani iweze kutekelezwa
Pia amesema kwa sehemu kubwa halmashauri hiyo inategemea mapato yake kutoka kwenye sekta ya uvuvi hivyo ni wajibu wa halmashauri kuhakikisha inasimamia vyema mapato hayo ili yasije kuingia kwenye mifuko ya watu wachache.
Aidha Katibu tawala amehimiza usimamizi wa maadili shuleni ili kuepusha mmomonyoko wa maadili kwa wanafunzi hasa masuala ya ushoga matumizi ya simu kwa wanafunzi wakati wa masomo miongoni mwa tabia zingine.