

20 June 2025, 6:44 pm
Miradi iliyotekelezwa katika kipindi cha miaka mitano ni katika sekta ya elimu, Afya, Maji, Umeme pamoja na Barabara
Na Adelinus Banenwa
Kata ya Manyamanyama, iliyopo katika Halmashauri ya Mji wa Bunda mkoani Mara, imepokea zaidi ya shilingi bilioni 2.28 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwa kipindi cha mwaka 2020 hadi 2025.
Akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa Kata ya Manyamanyama mbele ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM ya kata hiyo, Diwani wa Kata ya Manyamanyama, Mhe Mathayo Juma Machilu, amesema kuwa kiasi cha shilingi bilioni 2,282,809,000 kinatumika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika kata hiyo.
Mhe Machilu ameongeza kuwa miongoni mwa miradi iliyotekelezwa katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake ni katika sekta ya elimu ,Afya , Maji , Umeme pamoja na Barabara ikiwa vyanzo vya fedhi ni mapato ya ndani ya Halmashauri, Mfuko wa jimbo, nguvu za wananchi pamoja na serikali kuu.
Aidha Mhe Machilu amemshukuru Rais wa Jamuhuri ya muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kiasi kikubwa cha fedha kwa kata hiyo huku akiweka wazi kuwa atakwenda kutetea nafasi yake katika uchaguzi mkuu mwaka huu.
Awali akimkaribisha diwani kuzungumza na wajumbe wa halmashauri kuu ya CCM kata ya Manyamanyama mwenyekiti wa CCM kata ya Manyamanyama ndugu Masige Malegesi ambaye amesema haingekuwa busara kwa kwa diwani huyo aliyekabidhiwa ilani mwaka 2020 aondoke kinyemela ndiyo maana akaamu kikao hicho kuketi ili kujua yale waliyomuagiza ameyatekeleza kwa kiasi gani.
Ikumbukwe kwa mujibu wa tangazo la serikali kupitia kwa waziri mwenye dhamana na tawala za mikoa na serikali za mitaa Tamisemi ilitajwa kuwa ukomo wa mabaraza ya madiwani na udiwani ni tarehe 20 Juni 2025 ikiwa ni maandalizi kuelekea uchaguzi mkuu.