Mazingira FM

Kusaidia watoto wa kike ni kuunga mkono juhudi za serikali

5 June 2025, 3:35 pm

Wanafunzi wa shule ya sekondari ya Sazira wakifurahia baada ya kupokea msaada.

Mwalimu wa Malezi amesema kuwa msaada huo utasaidia kuinua mahudhurio na morali ya kitaaluma kwa wanafunzi wa kike.

Na Taro Michael Mujora

Katika kuunga mkono jitihada za kuinua elimu ya mtoto wa kike, Kanisa la PAGT Balili kwa kushirikiana na waumini wake limetoa jumla ya Pakiti 192 za taulo za kike kwa wanafunzi wa shule ya sekondari Sazira.

Wanafunzi wa shule ya sekondari ya Sazira wakifurahia baada ya kupokea msaada.

Mchungaji wa kanisa hilo Lenard Moto amesema kuwa msaada huo ni sehemu ya mchango wa kanisa katika kuhakikisha mtoto wa kike anasoma bila vikwazo vya hedhi, na ametumia fursa hiyo kuhamasisha taasisi na wadau wengine kuiga mfano huo kwa sababu jukumu la jamii ni kushirikiana na serikali kuboresha mazingira ya elimu, hasa kwa watoto wa kike Ili Hedhi isiwe sababu ya kukosa masomo.

Sauti ya Mchungaji Lenard Moto kutoka kanisa la PAGT

Wakizungumza na radio mazingira fm wanafunzi wa shule ya sekondari ya Sazira wamesema msaada huo utasaidia kuwa na utulivu wakati wa masomo kutokana na mwanzoni ilikuwa ikiwalazimu kutokuja shuleni kipindi ambacho wanakuwa kwenye hedhi.

Wanafunzi wa shule ya sekondari ya Sazira wakipokea msaada taulo za kike (pedi)

Elizabert Njogoro ambaye ni mwalimu wa malezi wa shule ya sekondari Sazira ameshukuru kwa msaada huo uliotolewa na kanisa la PAGT ambapo amesema utasaidia kupunguza changamoto ya mahudhurio na kuongeza morali ya kitaaluma kwa wanafunzi wa kike.

Sauti ya Elizabeth Njogoro