Mazingira FM
Mazingira FM
18 May 2026, 5:55 pm

Mradi huo ulipokea kiasi cha shilingi milioni 334 mwishoni mwa mwaka 2025 kwa ajili ya ujenzi.
Na Adelinus Banenwa
Baada ya Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Aswege Enock Kaminyoge, kutoa maelekezo ya ndani ya siku 14 kufunguliwa kwa Shule ya Msingi Victoria, shule hiyo hatimaye imeanza kutoa huduma rasmi leo Mei 18, 2026, kufuatia utekelezaji wa agizo hilo. Radio Mazingira FM ilitembelea eneo la shule hiyo na kubaini kuwa shughuli za masomo tayari zimeanza.

Akizungumza katika eneo la shule, Diwani wa Kata ya Nyasura, Magigi Samwel Kiboko, amesema kufunguliwa kwa shule hiyo ni hatua muhimu ya kupunguza msongamano wa wanafunzi katika Shule ya Msingi Nyasura, ambayo kwa muda mrefu ilikuwa ikikabiliwa na changamoto ya idadi kubwa ya wanafunzi. Amesema pia mradi huo ulipokea kiasi cha shilingi milioni 334 mwishoni mwa mwaka 2025 kwa ajili ya ujenzi.
Kwa upande wake, msimamizi wa mradi huo, Mwalimu Bernard Ngassa, amesema ujenzi wa shule hiyo ulianza mwezi Desemba 2025 na ulitarajiwa kukamilika ndani ya siku 90 sawa na miezi mitatu. Amesema mradi huo umehusisha ujenzi wa madarasa sita, jengo la utawala, madarasa mawili ya elimu ya awali pamoja na matundu 18 ya vyoo, na kwamba miundombinu yote hiyo imekamilika kwa wakati.

Mtendaji wa Kata ya Nyasura, Lezonia Mote, amesema baada ya kukamilika kwa shule hiyo kilichobaki ni kuhakikisha wanafunzi waliohamishiwa shule hiyo wanaendelea na masomo kwa kuwa sasa hivi hakuna kisingizio cha msongamano uliokuwepo awali katika Shule ya Msingi Nyasura.
Naye Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyasura C amesema mtaa umepokea kwa furaha ujenzi wa shule hiyo, na ameahidi kuhakikisha kunakuwa na ulinzi thabiti wa miundombinu ya shule pamoja na miradi mingine ya maendeleo iliyopo ndani ya eneo lake.