Mazingira FM
Mazingira FM
7 August 2026, 9:13 pm

Mkuu huyo wa Wilaya amesisitiza umuhimu wa kulinda vifaa vinavyotolewa na wadau wa maendeleo pamoja na Serikali, akieleza kuwa vifaa hivyo vinapaswa kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa ili viwanufaishe wananchi, hususan wanafunzi.
Na Adelinus Banenwa
Wito umetolewa kwa wadau mbalimbali wa maendeleo wenye nia ya kutoa misaada ya kimaendeleo ndani ya Wilaya ya Bunda, kufikisha misaada hiyo kwa Mkuu wa Wilaya au madiwani ili iweze kuwasilishwa na kugawanywa kwa kuzingatia mahitaji ya wananchi.
Wito huo umetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Mhe. Aswege Enock Kaminyoge, wakati akipokea kompyuta 10 zilizotolewa na Mbunge wa Afrika Mashariki, Mhe. Kambarage Wasira, ambazo zimewasilishwa leo katika ofisi yake.
Mhe. Kaminyoge amemshukuru Mhe. Kambarage kwa msaada huo, huku akiitaka Halmashauri kuhakikisha kompyuta hizo zinagawanywa kwa shule kwa kuzingatia mahitaji halisi, bila upendeleo.

Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya amesisitiza umuhimu wa kulinda vifaa vinavyotolewa na wadau wa maendeleo pamoja na Serikali, akieleza kuwa vifaa hivyo vinapaswa kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa ili viwanufaishe wananchi, hususan wanafunzi.
Kwa upande wake, Elly Mwabe, akizungumza kwa niaba ya Mhe. Kambarage Wasira, amesema kompyuta hizo zimetolewa kwa lengo la kusaidia kuongeza kiwango cha ufaulu katika shule za msingi na sekondari.
Mwabe amesema Mhe. Kambarage amedhamiria kuendelea na zoezi hilo la kutoa vifaa vya kielimu, ili kufikia halmashauri zote za Mkoa wa Mara na kusaidia kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.

Naye Katibu wa Uenezi wa CCM Wilaya ya Bunda Gasper Charles amesema chama hicho kinaunga mkono shughuli zinazofanywa na wawakilishi wa wananchi katika kuleta maendeleo.
Amesema wadau wanaochangia maendeleo wanapaswa kupewa ushirikiano, huku akimtaka Mkuu wa Wilaya pamoja na viongozi wa ngazi za chini kuhakikisha wanawapokea na kuwawezesha wadau wote wenye nia ya kuleta misaada na miradi ya maendeleo ndani ya Wilaya ya Bunda.