Mazingira FM
Mazingira FM
26 August 2026, 11:27 am

Watmetembezwa uchi porini, wengine wakaachiwa huku yeye akiendelea kushikiliwa na kufanyiwa vitendo vya ukatili. Akiwa huko, anasema alitishiwa kuuawa na kulazimishwa kumpigia simu mumewe pamoja na mama yake, akiwaomba watume shilingi laki tano. Mwanaume huyo alidai fedha hizo kuwa sharti la kumuachilia akiwa hai.
Na. Edward Lucas
Mwanamke mwenye umri wa miaka 18, ambaye jina lake limehifadhiwa, anadaiwa kutekwa na kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji, unyanyasaji na ukatili na mwanaume asiyefahamika, katika eneo la Mto Rubana, Kijiji cha Mihale, Kata ya Mcharo, Wilaya ya Bunda mkoani Mara.
Tukio hilo linadaiwa kutokea Agosti 22 mwaka huu, wakati mwanamke huyo alipokuwa mtoni akifua pamoja na wanawake wengine wawili.
Kwa mujibu wa maelezo yake, mwanaume huyo alifika eneo hilo akiwa pamoja na kijana mwingine, ikidai kuwa walikuwa wameingia katika eneo lililozuiliwa.
Mwanamke huyo anasema mwanaume huyo alianza kuwapiga na baadaye kuwafunga kamba, kabla ya kuwalazimisha kuingia porini.
Mwanamke huyo anaeleza kuwa wanawake wawili waliokuwa pamoja naye waliachiliwa na kuondoka, huku yeye akiendelea kushikiliwa na mwanaume huyo ambaye baadaye alidaiwa kumpeleka ndani zaidi ya pori.
Akiwa huko, anasema alitishiwa kuuawa na kulazimishwa kumpigia simu mume wake pamoja na mama yake, akiwaomba watume shilingi laki tano, huku mwanaume huyo akidai fedha hizo kama sharti la kumuachilia akiwa hai.
Mama wa mwanamke huyo, ambaye alitafutwa na Radio Mazingira Fm kwa njia ya simu juu ya tukio hili, amethibitisha kupokea simu kutoka kwa mwanawe na baadaye kuzungumza na mwanaume aliyedai kuwa amemshikilia mtoto wake.
Mama huyo amesema licha ya kutafuta fedha hizo, baadaye alipokea taarifa kutoka kwa watu waliokuwa wakimtafuta mwanamke huyo kwamba alikuwa ameokolewa na alikuwa tayari pamoja na askari.
Kwa upande mwingine, Mwenyekiti wa Mtaa wa Mihale, Manyama Magoiga, amesema alipata taarifa kuwa wanawake watatu walikuwa wameingizwa porini, ambapo wawili walifanikiwa kurudi, huku mmoja akiendelea kutoweka.
Mwenyekiti huyo amesema baada ya kuwasiliana na namba ya simu ya mwanamke huyo, ilipokelewa na mwanaume aliyetoa majibu yaliyokuwa na vitisho, hali iliyomfanya kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi Wilaya ya Bunda pamoja na askari wa uhifadhi.
Amesema askari na wananchi walishirikiana katika msako na hatimaye kumpata mwanamke huyo akiwa amefungwa kwenye mti, kabla ya kumpeleka hospitalini.
Hospitali ya DDH Bunda imethibitisha kumpokea mwanamke huyo Agosti 22 mwaka huu majira ya saa moja usiku akiwa na majeraha mbalimbali mwilini.
Supervisor wa hospitali hiyo, Livastus Benedicto, amesema mhanga alifanyiwa uchunguzi na vipimo mbalimbali, huku sampuli zikichukuliwa kwa ajili ya hatua zaidi za kitabibu na kisheria, na kupewa matibabu kulingana na hali yake.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mara limethibitisha kupokea taarifa ya tukio hilo na kusema linaendelea na jitihada za kuwabaini na kuwakamata watuhumiwa ili wafikishwe katika vyombo vya sheria.
Polisi pia limewataka wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi hilo kwa kutoa taarifa kuhusu watu wanaohusishwa au wanaoshukiwa kujihusisha na vitendo vya uhalifu, ili hatua stahiki zichukuliwe kwa wakati.