Mazingira FM

Wanafunzi wataja wazazi kuhusika na utoro wao shuleni

6 October 2026, 2:17 pm

Baadhi ya wanafunzi wameeleza kuwa wenzao hulazimika kubaki nyumbani kwenda shambani au kuchunga mifugo badala ya kuhudhuria masomo, huku uchelewaji na utoro vikiwa miongoni mwa changamoto zinazojitokeza.

Na Edward Lucas

Baadhi ya wanafunzi katika Shule ya Msingi Chingurubila wameeleza kuwa utoro unaojitokeza miongoni mwa wanafunzi unatokana na baadhi ya wazazi au walezi kuwazuia watoto kwenda shule kwa ajili ya kufanya shughuli za kilimo na ufugaji, hali inayoweza kuathiri haki yao ya kupata elimu.

Wakizungumza kuhusu changamoto zinazowakabili wanafunzi shuleni na nyumbani, wamesema baadhi ya wenzao hulazimika kubaki nyumbani kwenda shambani au kuchunga mifugo badala ya kuhudhuria masomo, huku uchelewaji na utoro vikiwa miongoni mwa changamoto zinazojitokeza.

Mwanafunzi Furaha Sayi Linda amesema changamoto hiyo inapobainika, wanafunzi hutoa taarifa shuleni ili walimu waweze kufuatilia na kuzungumza na wazazi pamoja na kuitisha vikao kwa lengo la kutafuta suluhisho huku mwanafunzi Joseph Manyama amesema wanafunzi pia hushirikiana katika kubaini wenzao wanaokosekana shuleni  .

Sauti ya Furaha Sayi Linda

Kwa upande wake, mwalimu wa Shule ya Msingi Chingurubila, Mwanahamisi Hassani, amesema shule imekuwa ikitumia walimu walezi na walimu wa madarasa kufuatilia mwenendo wa wanafunzi, ikiwemo utoro, ili kubaini mapema changamoto wanazopitia.

Amesema katika baadhi ya matukio, ufuatiliaji umebaini kuwa mwanafunzi amekosa shule kwa sababu amezuiwa ili kwenda shambani, kulima au kuchunga mifugo, jambo ambalo hulazimu shule kushirikiana na wazazi na jamii katika kutafuta suluhisho.

Sauti ya Mwanahamisi Hassani,

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Chingurubila, Nicolaus Ayaga, amesema shule imeweka mazingira ya shule salama kwa kuimarisha Dawati la Ulinzi wa Mtoto na ushirikiano kati ya walimu na wanafunzi ili kuhakikisha watoto wanalindwa wakiwa ndani na nje ya shule.

Amesema vikao vinavyohusisha shule, wazazi, serikali ya kijiji na kamati ya ulinzi na usalama vimekuwa vikisaidia kubaini na kushughulikia changamoto mbalimbali za ukatili dhidi ya watoto, ikiwemo ukatili wa kimwili, kingono, kisaikolojia na kihisia.

Sauti ya Nicolaus Ayaga

Hatua hizo zinaonyesha umuhimu wa ushirikiano kati ya shule, familia na jamii katika kubaini mapema dalili za ukatili dhidi ya watoto na kuhakikisha watoto wanapata fursa ya kuhudhuria shule, kusoma na kukua katika mazingira salama.