Mazingira FM
Mazingira FM
24 October 2026, 6:39 pm

Elimu hiyo inalenga kuwasaidia wananchi kuelewa haki na wajibu wao katika ndoa pamoja na taratibu za kisheria zinazopaswa kufuatwa pale wanapokabiliwa na migogoro inayoweza kusababisha kuvunjika kwa ndoa.
Na Adelinus Banenwa
Kunyimana haki ya tendo la ndoa, uzinzi, ukatili, kipigo, udhalilishaji na kutelekezana kwa muda mrefu ni miongoni mwa masuala yanayoweza kupelekea wanandoa kuomba talaka au mahakama kutoa talaka, kwa kuzingatia masharti ya sheria husika.
Akizungumza kuhusu suala hilo, Wakili Aloyce Kajitanus amesema kuna sababu mbalimbali zinazoweza kusababisha ndoa kuvunjika na kumfanya mmoja wa wanandoa kuchukua hatua za kisheria za kuomba talaka.
Wakili Kajitanus ameyasema hayo wakati akizungumza katika kipindi cha Ufahamu wa Sheria, kinachorushwa na Redio Mazingira FM, alipokuwa akitoa elimu kuhusu masuala ya ndoa na sababu zinazoweza kupelekea talaka.
Amezitaja sababu nyingine kuwa ni pamoja na kutengana kwa muda mrefu, kutelekezana kwa zaidi ya miaka mitano na mazingira yanayohusisha mmoja wa wanandoa kuhukumiwa kifungo cha maisha au kifungo cha miaka 30, kulingana na masharti ya sheria husika.

Aidha, elimu hiyo inalenga kuwasaidia wananchi kuelewa haki na wajibu wao katika ndoa pamoja na taratibu za kisheria zinazopaswa kufuatwa pale wanapokabiliwa na migogoro inayoweza kusababisha kuvunjika kwa ndoa.
Kupitia kipindi cha Ufahamu wa Sheria, kinachorushwa na Redio Mazingira FM, wananchi wanapata fursa ya kujifunza masuala mbalimbali ya sheria na kufahamu hatua zinazoweza kuchukuliwa katika kutatua changamoto zinazowakabili katika maisha ya kila siku.