Mazingira FM
Mazingira FM
21 September 2026, 10:08 am

Wakurugenzi wametakiwa kuhakikisha wanatenga fedha kwa ajili ya kugharamia mipango mbalimbali ya elimu ya watu wazima, ikiwemo kuwalipa walimu wanaofundisha wanafunzi wanaosoma nje ya mfumo rasmi, ili kuwapa motisha ya kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
Na Mariam Mramba
Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Aswege Enock Kaminyoge, amesema elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi ni miongoni mwa jitihada za Serikali kuhakikisha wananchi wote wanapata fursa ya elimu bila kujali umri, jinsia au mahitaji yao.
Kaminyoge amesema hayo wakati wa maadhimisho ya Juma la Elimu ya Watu Wazima na Elimu Nje ya Mfumo Rasmi, yaliyofanyika katika Shule ya Msingi Kisorya, Halmashauri ya Wilaya ya Bunda.
Katika maadhimisho hayo, Kaminyoge alimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mara, Brigedia Jenerali Evance Alfred Mtambi, ambaye alikuwa mgeni rasmi.
Amesema elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi ina umuhimu mkubwa katika maisha ya kila siku, kwa kuwa ni elimu isiyo na mwisho na inayomsaidia mwananchi katika nyanja mbalimbali.
Aidha, Mkuu huyo wa Wilaya ametoa wito kwa kila mmoja kushiriki kikamilifu katika kuhamasisha na kusimamia maendeleo ya elimu ya watu wazima na elimu nje ya mfumo rasmi.
Pia amewataka wakurugenzi kuhakikisha wanatenga fedha kwa ajili ya kugharamia mipango mbalimbali ya elimu ya watu wazima, ikiwemo kuwalipa walimu wanaofundisha wanafunzi wanaosoma nje ya mfumo rasmi, ili kuwapa motisha ya kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Akisoma taarifa , Afisa Elimu ya Watu Wazima na Nje ya Mfumo Rasmi, Bi. Florence Njiku, amesema takwimu zinaonesha kuwa Mkoa wa Mara una asilimia 14.1 ya watu wasiojua kusoma na kuandika.